Biblia inasemaje Kuhusu Mafundisho ya Injili ya Mafanikio?-2

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Mojawapo ya fundisho maarufu katika ukristo katika zama hizi ni injili ya mafaniko (prosperity gospel) au injili ya utajirisho. Injili hii inafundisha kuwa ukiwa mkristo mwaminifu una uhakika wa mafanikio kama vile utajiri, afya njema na kadhalika. Kwa mujibu wa mafundisho kuhusu njili ya mafanikio, mojawapo ya ishara kuwa wewe ni mwaminifu ni utoaji wa zaka za sadaka.

Wahubiri wanaofundisha juu ya injili ya mafanikio wamejipatia umaarufu mkubwa na wana wafuasi wengi  kutokana na ukweli kwamba kila mtu anapenda kuwa na mafanikio ya kifedha pamoja na afya njema na mafanikio mengine. Hata hivyo, baadhi ya watu wamekuwa wakipinga mafundisho juu ya injili ya mafanikio.

Kwa kuwa kuna pande mbili zinazopingana kuhusu injili ya mafanikio, mtu usipokuwa makini unaweza kuchanganyikiwa na usijue ukweli ni upi. Kwa kuwa msingi wa mafundisho ya dini ya kikristo ni Biblia, ni vizuri tuiulize Biblia kuhusu fundisho hili ili itueleze yenyewe. Hivyo katika makala haya, tutaangalia fundisho hili kwa mtazamo wa Biblia na siyo kwa maneno ya wahubiri.

Kupata makala ya nyuma inayofanana na hii, bonyeza hapa

Kabla hatujaanza kuangalia mafungu ya Biblia, hebu tujiulize swali hili, je, wakristo waaminifu hasa wanaotoa zaka na sadaka wote wana mafanikio ya kiuchumi na kiafya? Na je, watu wasio wakristo aua wakristo wasiotoa zaka na sadaka hawana mafanikio ya kiuchumi na kiafya? Bila shaka  kila mmoja naweza kupata jibu la swali hili kwa kuangalia watu wanaotuzunguka.

Uhalisia wa mambo ni kwamba kwamba mafanikio ya kiuchumi huwa si kwa wale wanaomwamini Mungu tu, maana hata waovu huwa wanapata mafanikio ya kiuchumi. Wakati mwingine, waovu wana mafanikio makubwa ya kiuchumi kuliko hata wacha Mungu.

Kwa kutambua kuwa hata waovu wanaweza kupata mafanikio ya kiuchumi, ndiyo maana wana wa Israeli walitangaza “Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao” (Malaki 3: 15).  Vilevile, Biblia inasema “Nami miguu yangu ilikuwa karibu na kupotoka, Hatua zangu zilikuwa karibu na kuteleza. Maana naliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki. Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na mwili wao una nguvu. Katika taabu ya watu hawamo, Wala hawapati mapigo pamoja na wanadamu. Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Jeuri huwavika kama nguo. Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao. Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu ……. Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki, Na kwa kustarehe siku zote wamepata mali nyingi. Hakika nimejisafisha moyo wangu bure, Nimenawa mikono yangu kwa kutokukosa. Maana mchana kutwa nimepigwa, Na kuadhibiwa kila asubuhi (Zaburi 73:2-8, 12-14).

Ukweli huu kuhusu mafanikio kwa waovu na kutokupata mafanikio kwa wenye haki uliwekwa wazi kwa mtunga Zaburi alipoingia patakatifu pa Mungu.” Nilipoingia patakatifu pa Mungu, Nikautafakari mwisho wao. Hakika Wewe huwaweka penye utelezi, Huwaangusha mpaka palipoharibika. Namna gani wamekuwa ukiwa mara!” Wametokomea na kutoweshwa kwa utisho (Zaburi 73:17).

Kwa upande wake, kitabu cha Malaki kinaelezea hatima ya waovu ni katika “siku iliyo kuu na kuogofya” (Malaki 4:5) ambayo inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi” (Malaki 4:1).

Kwa upande wa wenye haki hali itakuwa tofauti. “Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza-cheza kama ndama wa mazizini. Nanyi mtawakanyaga waovu; maana watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu; katika siku ile niifanyayo, asema Bwana wa majeshi (Malaki 4:2-3).

Pamoja na uwazi ulioko kwenye maandiko niliyoyanukuu hapa, bado baadhi ya wakristo wanang’ang’ania fundisho lisilo sahihi kuwa mtu akitoa zaka na sadaka kwa uaminifu ni lazima apate mafanikio ya kiuchumi.

Nikusihi uendelee kufuatilia makala haya ili tuweze kujifunza pamoja juu ya nini Biblia inasema kuhusu fundisho la injili ya mafanikio. Kwa kifupi ni kwamba fundisho hili ni sahihi lakini kwa namna linavyofundishwa, lina vitu vingi visivyo sahihi.. Tutaangalia mambo matano kuhusiana na Injili ya mafanikio ambayo yanapingana na mafundisho ya Biblia.

Ili usipitwe na makala kuhusiana na mada hii, endelea kufuatilia makala katika mtandao huu. Mtandao umesheheni makala nzuri  kuhusu masuala mbalimbali kama vile mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto, fedha, biashara na uwekezaji.

Ili usikose makala zinazoandikwa katika mtandao huu, unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala hizo mojawa kwa moja kwenye email yako kila zinapowekwa mtandaoni.

Ili uweze kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

1 comment / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *