Biblia Inasemaje Kuhusu Injili ya Mafanikio?- 3

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Karibu katika sehemu ya tatu ya mfululizo wa makala kuhusu injili ya mafanikio ambapo tunaangalia Biblia inasemaje kuhusu injili hiyo. Leo, tutaona namna ambavyo injili ya mafanikio inavyopotosha tabia ya Mungu kuhusu upendo na namna ambavyo injili hiyo inamfanya mwanadamu awe kiumbe cha kufikirika tu. Karibu tujifunze pamoja.

Kupata makala ya nyuma kuhusu mada hii bonyeza hapa

Injili ya mafanikio inapotosha tabia ya Mungu kuhusu Upendo

Maandiko matakatifu hufunua tabia ya Mungu ya upendo kwa watu wote. Mungu ni mwingi wa rehema hata kwa wanaomchukia. Biblia inaeleza kuwa Mungu aliupenda ulimwengu kiasi cha kumtoa mwanaye wa pekee ili kila amwaniye apate uzima wa milele (Yohana 3:16). Mungu aliamua kumtoa mwanaye wakati wanadamu tulikuwa tungali wenye dhambi na maadui wa Mungu (Warumi 5:8, 10).

Mungu bado anawapenda wanadamu bila kujali hali ya kimaadili waliyofikia kama athari ya dhambi. Katika Mathayo 5:45, Neno la Mungu linasema “maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”. Pamoja na kwamba Mungu ni moto ulao (Waebrania 12:29) kwa dhambi, lakini hapendi mtu yeyote apotee bali wote wafikilie toba (2 Petro 3:9). Yesu ambaye ni Mungu aliwapenda hata maadui zake kiasi cha kuwasamamehe waliomsulubisha (Luka 23:34).

Kufundisha kwamba Mungu anawapatia mafanikio wale tu wanaomwamini na wale tu wanaotoa zaka na sadaka ni sawa na kufundisha kuwa Mungu wetu ni Mungu mwenye upendeleo. Injili ya mafanikio inamfanya Mungu aonekane kama Mungu anayejali zaidi kupata fedha na mali zingine kutoka kwa waumini wake kuliko Mungu anayetaka watu waishi kwa kila Neno litokalo katika kinywa chake (Mathayo 4:4). Injili ya mafanikio inawafanya waumini wawe kama wafanyabiashara wa fedha (wakopeshaji) ambao wanatoa fedha zao kwa Mungu wakitegemea kupata fedha zao pamoja na “riba”. Hii si tabia halisi ya Mungu amabye habari zake tunazisoma kwenye Bibilia, labda kama kuna Mungu mwingine tofauti na huyu.

Injili ya mafanikio inaufanya uwepo wa wanadamu uwe wa kufikirika zaidi

Wanadamu wote sasa wako katika pambano kuu kati ya Kristo na Shetani kuhusu tabia ya Mungu, Sheria yake na utawala wake juu ya Ulimwengu. Hili ni pambano kati ya wema na uovu. Historia ya pambano kuu, imepitia mchakato mrefu ambayo ilianzia na anguko la mwanadamu pale Edeni na itaishia na urejeshwaji upya wa uhusiano wa mwanadamu na Mungu katika nchi mpya na mbingu mpya. Tangu Edeni kumekuwa na pambano kati ya nguvu za Mungu na nguvu za uovu.

Akiandika juu ya pambano hili, Mtume Paulo anasema “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” (Waefeso 6:12). Yesu mwenyewe alitangaza kuwa mawakala wa shetani “watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule” (Mathayo 24:24).

Katika maandiko, shetani anatajwa kama “baba wa uongo” (Yohana 8:44) na mshitaki wa ndugu zetu (Ufunuo 12:10) na pia hufanya kila awezalo kuleta mateso kwa wanadamu wakiwemo wanaomwamini. Mfano halisi wa mtu aliyepata mateso kutoka kwa shetani ni Ayubu. Licha ya kuwa mcha Mungu, mnyoofu na mwelekevu wa moyo lakini alipitia mateso na kupoteza watoto na mali zake. Ayubu alipata haya si kwa sababu ya dhambi bali ili jina la Bwana litukuzwe (Ayubu 2).

Katika agano jipya, kuna siku Yesu alikutana na mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa kwake. “Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake (Yohana 9:2-3).

Upo ushahidi ulio wazi kutoka ndani na nje ya Biblia wa watu wanaomwamini Yesu lakini walipitia katika changamoto nyingi na maisha ya shida. Yesu mwenyewe alizaliwa katika mazingira ya shida (Mathayo 8:20; Luka 9:58). Kama kweli, Mungu anawapatia utajiri watu wote wanaomwamini, kwa nini hakumpatia utajiri mwanaye Yesu na akamuacha bila hata mahali pa kulaza kichwa chake (Mathayo 8:20, Luka 9:58).

Je, kwa nini Mungu hakuwapatia utajiri mitume?  Petro alitangaza mwenyewe kuwa hakuwa tajiri (Matendo 3:6).  Kwa upande wake mtume Paulo alijitahidi kutokuwa mzigo kwa waumini katika safari zake za kuhubiri injili lakini bado hakuwa na uwezo wa kujihudumia mahitaji yake yote na ilibidi apate msaada wa mahitaji yake kutoka kwa waumini (2 Wakorintho 11: 9).

Biblia inaeleza sifa mojawapo ya kanisa la mitume ni “kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja” (Matendo 2:45). Hii inadhihirisha kuwa baadhi ya waumini walikuwa maskini kiasi cha kusaidiwa na waumini wenzao.  Sasa swali la kujiuliza ni hili: Mungu wa injili ya mafanikio ni tofauti na Mungu wa Agano la kale na Mungu wa kanisa la awali?

Kwa bahati nzuri, Biblia iko wazi katika hili maana Mungu mwenyewe anasema “Kwa kuwa mimi, Bwana sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo” (Malaki 3:6). Kwa Mungu hana kigeugeu, Mungu wa Agano la Kale ni yuleyule wa Agano jipya, likiwemo kanisa la awali na kanisa la leo.

Baadhi ya wahubiri wa injili ya mafanikio hufundisha kuwa kila jambo baya huwa linasababishwa na mapepo. Kwa mfano, wanadai kuwa magonjwa na umaskini husababishwa na mapepo na ili mtu apone au aondokane na umaskini ni lazima mapepo hayo yakemewe. Ni kweli kwamba magonjwa na mateso ya aina yoyote hayakuwa sehemu ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Hata hivyo, ukemeaji wa mapepo unapofundishwa katika injili ya mafanikio unaifanya injili hiyo iwe injili bila msalaba wa Kristo (Mathayo 10:38; 16:24, Marko 8:34, Luka 9:23; 14:27). Kama muumini anapaswa kuishi bila matatizo, kwa nini Paulo aliishi na mwiba katika mwili wake? (2 Wakorintho 12:7-10). Isitoshe, fundisho kwamba kila jambo baya linatokana na mapepo halipatikani popote katika Biblia.

Maandiko matakatifu yakisomwa katika muktadha wake sahihi, yanaeleza wazi kuwa pambano na nguvu za giza halitakoma kwa wakristo wakati tukiwa katika ulimwengu huu wenye shida na dhambi (Waefeso 6:10–18; 1 Petro 5:8, 9). Kwa hiyo, si sahihi kufundisha kuwa ukimwamini Yesu matatizo yako yote yataisha maana Yesu mwenyewe alisema kuwa wafuasi wake watakutana na changamoto mbalimbali katika maisha yao (Mathayo 10:34–39). Mtume Paulo naye alieleza “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa” (2 Timotheo 3:12). Kimsingi, Bwana wetu Yesu Kristo hakuahidi kuwa ataondoa matatizo katika maisha ya wote wanaomwamini (Mathayo 8:23–27; Marko 4:35–41; Luka 8:22–25). Hivyo, changamoto za maisha ikiwemo magonjwa na umaskini ni sehemu ya pambano kuu na si lazima zisababishwe na kukosa uaminifu kwa Mungu ikwemo kutotoa zaka na sadaka.

Je, unapenda kupata mafunzo endelevu kutoka katika mtandao huu?

Ili uweze kupata makala kuhusu mada hii na mada zingine kuhusu mafanikio, jiunge na mtandao huu. Kwa kufanya hivyo, utaweza  kupata makala hizo moja kwa moja kwenye email yako kila zinapowekwa mtandaoni. Mtandao huu unatoa mafunzo endelevu kuhusu mafanikio hususani kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto na mambo mengine mengi ya kiroho.

Ili uweze kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

1 comment / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *