Unajua Fedha Zako Zinaenda Wapi?

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kuna vitu huwa vinamshangaza kwenye matumizi ya fedha. Kwanza, akipata fedha, huwa huwa hahangaiki kukaa chini na kupanga azitumieje lakini zinapoisha tu ndipo mawazo na mipango mizuri huwa inamjia akilini mwake. Wakati bado fedha hizo zipo mipango hiyo huwa haiji akilini. Pili, huwa hawezi kueleza fedha zake zimeishaje au zimeenda katika matumizi yapi? Anachofahamu tu ni kwamba fedha zake hazipo. Wengi, tuko kama huyu rafiki yangu.Tunatumia fedha na zikiisha huwa hatuwezi kujua zimeishaje!!

have no money, isolated on white background.

Mojawapo ya changamoto inayowakabili wengi katika kudhibiti matumizi yao ya fedha ni kutojua fedha yao inakwenda wapi. Ukimuuliza mtu yeyote akueleze, kwa mfano, anatumia kiasi gani cha fedha kwa mwezi kwa ajili ya chakula, vocha za simu, usafiri, starehe na kadhalika bila shaka wengi watashindwa kukujibu. Kutokujua unatumia kiasi gani cha fedha kwa ajili ya kitu fulani ndiyo chanzo cha kukosa nidhamu ya matumizi. Matokeo yake watu wengi huwa wanashangaa tu fedha yao imeisha huku wakiwa na mahitaji mengi ambayo yanahitaji fedha. Katika hali hii, ni vigumu kuamua utadhibiti vipi matumizi yako.

Kabla ya kuamua kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha, ni vizuri ufahamu unatumia kiasi gani cha fedha kwa kitu gani. Unaweza kufanya hivyo kwa kuanza kufuatilia matumizi yako kwa siku, wiki na mwezi. Ili uweze kufuatilia matumii hayo, unaweza kuorodhesha matumizi yako ya kila siku kwa kipindi cha mwezi mzima. Orodhesha kila matumizi yako bila kujali ni matumizi madogo kiasi gani na mwisho wa mwezi utaweza kujumlisha matumizi hayo na kupata picha unatumia kiasi gani cha fedha kwa kitu gani. Taarifa hizi zitakusaidia kuamua urekebishe wapi na pia itakuwezesha kuandaa bajeti yako ya kipindi fulani.

Upangaji wa bajeti utakusaidia kujua maeneo muhimu ya kuyapa kipaumbele na kutunza pesa kwa ajili ya dharura au mipango yako ya baadaye ya maendeleo. Watu wengi wanaingia katika matatizo au kutokujua pesa yao inatumikaje kwa sababu hawana utaratibu wa kupanga bajeti.

Nini maana ya bajeti?

Kwa kifupi, bajeti ni mpango wa kifedha unaonyesha makadirio ya mapato na matumizi katika mradi, biashara, mtu binafsi, taasisi au serikali ndani ya kipindi fulani. Kipindi hicho kinaweza kuwa siku, wiki, mwezi au mwaka.  Vipengele muhimu katika bajeti ambavyo unapaswa kuvifanyia kazi ni mapato na matumizi. Hivyo, bajeti inaonyesha makadiro ya mapato ndani ya kipindi fulani pamoja na makadirio ya matumizi ndani ya kipindi hicho.

Bajeti ni kitu cha muhimu sana kwa mtu yeyote anayetaka kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kufikia utajiri na uhuru wa kifedha. Pamoja na umuhimu wa kupanga bajeti,  watu wengi hawapendi kuandaa bajeti kwa sababu wanadhani itawabana kuishi kama wapendavyo. Wengine wanadhani kuwa wanaotakiwa kupanga bajeti ni wale wenye kipato kikubwa tu. Lakini ukweli ni kwamba bajeti ni kwa ajili ya watu wote bila kujali kipato chao. Bajeti inasaidia mtu kuishi kulingana na kipato chake, yaani mapato kuwa makubwa kuliko matumizi.

Kwa nini upange bajeti?

Maandiko Matakatifu yanasisitiza umuhimu wa kupanga kabla ya kuanza utekelezaji wa jambo lolote. Bwana wetu Yesu Kristo alieleza vizuri suala hili kwa kutumia mfano wa ujenzi wa mnara. “Maana ni nani kati ya ninyi kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kumalizia? Asije akashindwa kumalizia baada ya kupiga msingi watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema mtu huyu alianza kujenga akawa hana nguvu ya kumalizia” (Luka 14:28-30). Kisa hki kinatufundisha kuwa mtu yeyote aliye makini katika matumizi ya fedha  anapaswa kuweka mipango mizuri kabla ya kuanza kutumia fedha yake. Njia ya kuweka mipango hiyo ni kupitia bajeti.

Baadhi ya faida za kuwa na bajeti kwa mtu binafsi au familia ni kama ifuatavyo:

1. Bajeti inakusaidia kudhibiti matumizi yako na kuepukana na matumizi yasiyo ya lazima. Kupanga bajeti ni moja ya mkakati madhubuti unaoweza kukusaidia kubana matumizi na kuielekeza pesa yako katika mambo muhimu. Kwa hiyo, upangaji wa bajeti na kuishi kwa bajeti kwa ujumla itakusaidia kuwa na nidhamu inayoleta maendeleo katika shughuli zako na maisha kwa ujumla.

2. Bajeti inakurahisishia kuweka akiba ya kipato chako kwa kuwa upangaji wa bajeti unakuondolea tabia ya kutumia kipato chako chote au kutumia zaidi ya kipato chako. Kuweka akiba kunasaidia kupata fedha ya biashara na uwekezaji. Akiba pia inaweza kukusaidia wakati unapopata dharura.

4. Bajeti itakusaidia kuepukana na maisha ya starehe na anasa. Starehe si tu kwenda kwenye kumbi za starehe kama vile klabu, dansi na baa, bali pia maisha ya nyumbani kama vile kununua vitu vingi na vya gharama kubwa ambavyo kimsingi havikusaidii kukua kiuchumi kama vile radio kubwa, televisheni kubwa na ya bei ya juu, simu ya bei ya juu, magari ya kifahari na kadhalika. Kwa hiyo, bajeti yako itakusaidia sana ikiwa pesa nyingi na mipango yako mingi imeelekezwa kwenye maeneo yanayokupatia kipato.

5. Bajeti inaweza kukusaidia kujua uwezo wako wa kifedha. Unapopanga bajeti, unaweza kujua kipi unamudu kufanya na kipi hautamudu kulingana na kipato chako. Hii inaweza kukupatia hamasa ya kuongeza kipato chako ili uweze kumudu mahitaji mbalimbali ya kifedha ambayo kwa sasa huwezi kuyamudu.

Unapangaji wa bajeti hufanyikaje?

Uandaaji wa bajeti binafsi au ya familia siyo kitu kigumu na unaweza kufanya wewe mwenyewe bila hata usaidizi wa mtaalam wa mambo ya fedha ili mradi. Kwa bajeti yako binafsi, unaweza kupanga bajeti yako kwa mwezi. Lakini unaweza kuchagua kipindi kingine kutegemeana na chanzo na mtiririko wa kipato chako. Zipo hatua kadhaa unazopaswa kufuata katika kupanga bajeti yako.

Je, ungependa kufahamua hatua hizo? Hatua hizo zimeelezwa kwa kina katika kitabu kiitwacho: SIRI ZA MAFANIKIO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi na Kukabiliana na Migogoro na Changamoto za Kifedha Katika Ndoa na Familia.

Pamoja na mambo mengine,katika kitabu hiki utaweza kufahamu hatua kwa hatua namna ya kuanda bajeti yako.

Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kuhusu kitabu kitabu bonyeza hapa.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio.Kupitia mtandao huu utaweza kupata makala mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kujiunga na matandao huu, utaweza kupata makala kupitia email yako mojakwa moja kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga jaza fomu iliyok hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

1 comment / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *