Rafiki yangu Mpendwa katika Krsito,
Kuanzia ijumaa ya wiki iliyopita (Julai 22, 2020) kuliibuka taharuki na na mijadala mikali iliyojaa malalamiko kutoka watumishi wa umma. Kilichosababisha taharuki na mjadala ni ongezeko la mshahara. Kama hukusikia chchocte kuhusu taharuki hiyo unaweza kushangaa kwamba inakuwaje watu waongezewe mshahara halafu wapate taharuki na waibuke na malalamiko badala ya kushangilia. Kilichoibua taharuki ni nyongeza ya mshahara ambayo haiendani na matarajio ya watumishi wa umma. Walitegmea ongezeko kubwa lakini wamepata ongezeko dogo sana.
Pengine kilichowaumiza zaidi ni kwamba, wamekaa kwa miaka sita mfululizo bila kupata nyongeza yoyote ikiwa ni tofauti kabisa na utamaduni ulizoeleka huko nyuma kwamba kila mwaka walikuwa wanapata ongezeko la mshahara kuanzia Julai mosi ya kila mwaka. Baada ya kukaa kwa miaka yote hiyo bila ongezeko la mshahara walitegmea kuwa watapata ongezeko kubwa la kufidia maumivu walioyapta kwa miaka sita mfululizo.
Hakika, kuna mambo mengi tuyoweza kujifunza kutoka katika tukio hili. Moja kati ya hayo ni namna ilivyo hatari kutegmea mshahara kama njia ya kujipatia mafanikio ya kifedha. Sitaki kuhukumu, lakini wengi waliolamikia nyongeza ndogo ya mshahara ni wale ambao mshahara ndiyo tegemeo lako kuu katika mafanikio ya kiuchumi. Wangekuwa na vyanzo vingine vya kipato wala wasingejali sana ongezeko hilo. Hivyo,taharuki iliyotokea iwafundishe waajiriwa kuwa na vyanzo vingine vya kipato zaidi ya mshahara.
Kwa bahati mbaya sana, katika jamii zetu, mshahara ndiyo njia ya kujipatia kipato inayoheshimika kuliko njia zingine. Vilevile, kundi wa waajiriwa ni kundi la watu linaloheshimika sana katika jamii kutokana na sababu mbalimbali. Sababu mojawapo hiyo niliyoitaja kwamba ni watu wanaopata mashahra , hivyo wana uahakika wa kipato na maisha mazuri kuliko watu wengi.
Sababu nyingine ni kwamba waaajiriwa wengi ni wasomi, yaani watu wenye elimu kubwa ya darasani na elimu hiyo ndiyo inawafanya waonekane wa maana na waheshimike. Kwa kawaid, kila msomi anataka kuajiriwa kwa sababu mfumo wa elimu umemuandaa kuajiriwa. Hali hii imepelekea jamii iamini kuwa watu walioshindwa kupata elimu ya darasani ndiyo wanapaswa kufanya shughuli zingine za kujipatia kipato kama vile kumiliki biashara ndogo na kubwa na uwekezaji. Hata hivyo, ukweli ni kwamba ajira haiwezi kumpatia mtu utajiri na uhuru wa kifedha.
Kwa nini ajira haiwezi kukupatia mafanikio ya kifedha?
Ajira pekee haiwezi kumfanya mtu awe tajiri na huru kifedha kwa sababu zifuatazo:
- Kipato anacholipwa mwajiriwa ni kidogo: Upo ukweli ambao haufahamiki kwa watu wengi kuhusu mshahara. Ukweli huo ni kwamba hakuna mwajiri mahali popote duniani aliye tayari kukulipa mshahara utakaokufanya kuwa tajiri au huru kifedha. Mishahara hata inayoonekana kuwa mikubwa ni kwa ajili ya kukuwezesha kupata mahitaji yako ya muhimu tu kama vile chakula, makazi/malazi, mavazi, matibabu, elimu ya watoto na mahitaji mengine muhimu. Waajiri hawawezi kutoa mshahara wa kukuwezesha kuwa kuwa huru kifedha kwa sababu mbili kuu. Kwanza, waajiri wengi wako kibiashara zaidi na wanalazimika kukulipa kidogo ili wabakiwe na faida.
Hata waajiri ambao si wafanya biashara kama vile serikali na mashirika yasiyo ya faida (not for profit organizations) wana mambo mengine muhimu yanayohitaji fedha kama vile hutoa huduma kwa wananchi. Hivyo, wanalazimika kukulipa mshahara kidogo ili fedha zingine zielekezwe katika kutekeleza majukumu yao mengine. Kwa mfano, kwa sasa Serikali ya Tanzania inatekeleza miradi mingi ya kimkakati mabyo inahitaji fedha nyingi sana. Miradi hiyo ni pamoja na ujezni wa reli ya mwendo kasi, mradi wa umeme wa maji wa Mwalimu Nyerere (Nyerere hydropower project), miundombinu ya barabara, ununuzi wa ndege na kadhalika. Miradi hii ndiyi imesababusha watumishi wa umma wasiongezewe mishahara kwa miaka sita mfululizo. Kama Serikali itaamua kuongeza mishahara mikubwa kwa watumishi wake, miradi hii itachukua muda mrefu sana kukamilika.
Sababu ya pili ni kwamba waajiri wanalazimikia kukulipa mshahara mdogo ili uendelee kuwategemea na hivyo uendelee kufanya kazi. Kama watakulipa mshahara mkubwa na kuwa huru kifedhai unaweza kuacha kazi na hivyo wakakosa huduma yako. Kutokana na sababu hizi, mwajiriwa yeyote anayetegemea mshahara kama chanzo pekee cha kipato hata kama anapata mshahara mkubwa kiasi gani hawezi kupata uhuru wa kifedha bali ataishia tu kuwa maskini au mtu mwenye kipato cha kati.
- Mwajiriwa hana uamuzi wa mwisho juu ya kipato chake. Kipato cha mwajiriwa ni mshahara na kwa kawaida, mwajiri ndiye hupanga mshahara wa mwajiriwa na hata pale ambapo kuna fursa ya majadiliano ya mshahara mwenye uamuzi wa mwisho ni mwajiri. Kwa hiyo, mwajiriwa hupokea kile anachoamua mwajiri hata kama hakimtoshi. Hata pale uzalishaji unapoongezeka kazini au faida inapoongezeka, si lazima mshahara nao uongezeke.
- Waajiriwa wengi wana maisha ya kuiga: Waajiriwa wengi wanaishi maisha yasiyoendana na kipato chao. Wengi wamejitengenezea maisha ya aina fulani kiasi kwamba kila mwajiriwa wa ofisi fulani au ngazi fulani huwa anataka aishi maisha ya aina hiyo. Kwa mfano, waajiriwa wengi wenye digrii siku hizi wanaendesha magari na imekuwa kawaida kila mwenye digrii kufanya kila awezalo ili kuwa na gari kwa lengo la kufanana na wenzake katika ofisi anayofanya kazi au aliosoma nao chuoni. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa wengi hawana uwezo wa kumiliki gari kutokana na kulipwa mshahara mdogo. Ili kumudu kununua gari wanalazimika kuingia katika mikopo na kuishia kuishi maisha magumu bila sababu.
- Uhakika wa kipato unawafanya wasijishughulishe kuongeza kipato: Kwa kuwa waajiriwa wana uhakika wa kipato kila mwezi, hubweteka na kushindwa kutafuta vyanzo vingine vya kipato. Lakini kwa mfanyabiashara au mtu aliyejiajiri hulazimika kujishughulisha zaidi ili kujihakikishia uhakika wa kipato. Vilevile, wasio waajiriwa hulazimika kuwa na vyanzo vingi vya kipato ili chanzo kimoja kisipofanya vizuri basi waweze kuendelea kupata kipato kutoka katika vyanzo vingine.
- Jamii ina matarajio makubwa kutoka kwa waajiriwa: Kama ambavyo nimeeleza awali, jamii zetu zina mtazamo kuwa waajiriwa wana uwezo mkubwa wa kifedha na wana uhakika wa kipato. Mtazamo huu unawafanya watu wengi wawategemee waajiriwa kifedha bila kujali hali halisi ya uwezo wao. Matokeo yake, waajiriwa wengi wanatumia pesa nyingi kusaidia ndugu, jamaa, marafiki na jamii kwa ujumla na kujikuta wao wenyewe wanaishi maisha magumu.
- Waajiriwa wengi hawana elimu ya fedha: Kwa kuwa elimu mfumo wetu wa elimu inawaandaa watu kuwa waajiriwa, elimu ya usimamizi wa fedha binafsi huwa haifundishwi katika elimu ya darasani. Kwa sababu hiyo waajiriwa wengi hawana maarifa ya namna ya kupata fedha, kuisimamia na kuiongeza na wanabaki kutegemea mshahara tu ambao hauwezi kuwasaidia kufikia uhru wa kifedha maana hata namna ya kupangilia tu matumizi ya mshahara huo hawajui.
Kwa bahati mbaya sana, wengi wa wasomi na wa elimu ya darasani hawajui kwamba hawana elimu fedha na hivyo hawahangaiki kuitafuta. Hata wale ambao wamesoma masomo ambayo yanahusu usimamizi wa raslimali fedha kama vile uhasibu, uchumi, biashara na kadhalika, nao elimu yao inawaandaa kusimamia fedha za wengine( Serikali,mashirika n.k) na siyo fedha zao.
Kutokana na ombwe na elimu ya fedha lililopo katika mfumo wetu wa elimu, kuna haja ya kutafuta elimu hiyo nje ya mfumo rasmi wa elimu . Njia mojawapo ya kupata elimu hiyo ni kujisomea vitabu vizuri kuhusu elimu ya msingi ya fedha. Mojawapo ya vitabu hivyo ni kitabu kiitwacho :
SIRI ZA MAFANIKIO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi na Kukabiliana na Migogoro na Changamoto za Kifedha Katika Ndoa na Familia.
Hiki ni kitabu cha muhimu sana kwa yeyote anayetaka kujifunza elimu ya fedha ambayo haifundishwi darasani.
Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kuhusu kitabu kitabu bonyeza hapa.