Hivi Ndivyo Unavyoweza Kumjua Mchumba Anayekupenda Kwa Dhati

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Watu wengi wanaotafuta wachumba au walioko kwenye uchumba huwa wanajiuliza, nitawezaje kumjua mchumba mwenye mapenzi ya dhati kwangu na nitawezaje kumbaini yule asiye na mapenzi ya dhati kwangu? Kila mtu anayetafuta mchumba au aliyeko kwenye uchumba tayari, ni muhimu sana kujiuliza maswali hayo. Usipojiuliza maswali haya na kupata majibu yake unaweza ukajikuta unatumbukia kwenye mikono ya matapeli wa mapenzi, yaani mtu asiye na mapenzi ya dhati kwako na ukaja kujuta baadaye.

Kimsingi, maswali hayo ni magumu sana na yanaweza yasiwe na majibu rahisi na ya moja kwa moja. Hata hivyo katika makala haya, nitakushirikisha njia ambayo unaweza kuitumia kama kigezo cha kumpima mchumba mwenye mapenzi ya dhati kwako. Njia hiyo ni kuangalia tabia na matendo yake kwako.

 Yafuatayo ni mambo unayoweza kuyatumia kuthibitisha kuwa mchumba wako anakupenda kwa dhati au la.

1.      Uwazi

Mchumba anayekupenda kwa dhati na aliyeamua kikwelikweli kuwa mwenzi wako wa maisha, atakuwa muwazi na huru kukueleza au kukushirikisha mambo yake yote. Mtu huyo daima hataona ugumu kufunguka kwako kuhusu hisia zake, mawazo yake, kile anachokipenda, mambo asiyoyapenda, historia yake na hata matatizo yake binafsi. Ukiona anafanya hivyo ni ishara kuwa anakupenda na anatambua kuwa wewe ni sehemu yake na hivyo unapaswa kujua chochote kinachomhusu yakiwemo mambo yake ya siri.

Ikitokea una mchumba ambaye kila kitu kumhusu yeye ni siri, basi huenda hana mpango na wewe bali anakupotezea muda tu. Wakati mwingine, anaweza kukueleza mambo yake baada tu ya wewe kutumia nguvu nyingi sana. Hapa napo kuna tatizo. Uwazi si suala la kutumia nguvu bali ni kitu kinachokuja chenyewe tu.

2.      Ukaribu

Mtu anayekupenda atatamani kuwa karibu na wewe wakati wote. Ukaribu unaweza kuwa wa kuonana mara kwa mara na kutumia muda pamoja au mawasiliano kwa njia mbalimbali kama vile simu pale ambapo hamuwezi kuonana. Kama mchumba wako anakukumbuka kwakupiga simu au  kukutumia ujumbe wa maneno kupitia simu yake, kukutumia barua pepe, kuchati na wewe mara kwa mara unapokuwa mbali naye hali akijaribu kukueleza jinsi alivyo kukumbuka, hiyo ni dalili kwamba anakupenda na anakuona wewe ni mtu wa muhimu sana kwake.

Ikitokea mchumba wako haoni umuhimu wa kuwa karibu na wewe, ni dalili mbaya kwamba huenda hakupendi. Kwa mfano, kama mnaishi katika mji mmoja lakini hafanyi jitihada yoyote ya kukutafuta ili muweze kukutana au kama yuko mbali lakini hana bidii ya kuwasiliana na wewe ni dalili mbaya. Sio lazima akupigie simu kiasi cha kukufanya usifanye kazi zako ndio ujue kuwa anakupenda. Kumbuka kuwa ana majukumu pia, hivyo kama na wewe unampenda zingatia uwiano wa mapenzi yenu na kazi. Hebu chukua muda jiulize, je wewe na yeye nani ana kawaida ya kuanzisha mawasiliano mara kwa mara. Kwa mfano, nani huwa anapiga simu mara kwa mara? Nani huwa anaandika meseji mara kwa mara? Kama ukiona wewe ndiyo unamtafuta mara kwa mara kuliko yeye anavyokutafuta basi ujue hapo kuna tatizo.

3.    Kukujali wakati wa shida

Baadhi ya watu huwa wako karibu na mtu mwingine pale wanapokuwa katika hali nzuri. Yaani hawana matatizo yoyote lakini inapotokea unapata matatizo fulani kama vile ugonjwa, msiba  hali ngumu ya kiuchumi wanakaa mbali na wewe. Je, unapokuwa na huzuni na unahitaji faraja ya ukaribu au unapokuwa mgonjwa, mchumba wako huwa yupo tayari kutenga muda wake kwa ajili yako? 

Ikitokea mchumba wako hajakujali wakati wa matatizo wakati angewezea kufanya hivyo basi huyo hana upendo wa dhati kwako. Kumbuka mtakapokuwa katika ndoa, mume wako au mke wako ndiyo msaada namba moja pale unapopata changamoto au tatizo lolote. Sasa kama wakati wa uchumba hajaonesha kukujali, itakuwaje wakati mtakapokuwa kwenye ndoa? Ndiyo maana katika kiapo cha ndoa kuna maneno yanayowataka wanandoa kuahidi kuwa watakuwa pamoja katika shida na raha. Kama hawezi kuwa pamoja na wewe katika shida wakati wa uchumba, hata kama ataahidi kwa kiapo kuwa atakuwa na wewe, inaweza kuwa ahadi ya mdomoni tu na siyo ya vitendo.

4.      Anapenda fedha

Fedha ni muhimu sana katika maisha na kila mtu anapaswa kufanya bidii kuwa na fedha ya kutosha ili awe na maisha mazuri. Pamoja na ukweli huu, wapo watu ambao wanapenda fedha kuliko kupenda watu. Watu wa aina hiyo, hata wanapotaka kutafuta mwenzi wa maisha huangalia zaidi uwezo wake wa kifedha na siyo mambo mengine. Ukipata mwenzi wa ndoa wa aina hiyo, ujue tu kwamba siku ukijikuta umeishiwa, fedha unaweza kuwa ndiyo mwisho wa mahusiano yenu. Hivyo, unapaswa kuwatambua watu wa ina hiyo na kuwa nao makini mapema wakati wa uchumba.

Sasa utawezaje kujua kuwa mchumba wako anapenda fedha zako zaidi kuliko kukupenda wewe? Kuna namna nyingi za kuweza kumtambua mtu wa aina hiyo. Namna mojawapo ni kupitia mazungumzo yake. Watu wa aina hiyo wanapenda sana kuzungumzia fedha. Kwa mfano, mojawapo ya mambo ya kwanza kabisa kukuuliza ili akufahamu zaidi ni kuhusu fedha. Baadhi ya maswali anayoweza kukuuliza ni haya ni kuhusu kazi yako na kipato chako, kama una gari, una nyumba au umepanga, una miradi gani ya kukuingizia kipato, kama unafanya biashara atataka kujua mtaji wako ni kiasi gani. Kwa kifupi anapenda kuuliza maswali yatakayomsaidia kujua uwezo wako wa kifedha.

Unaweza pia kujua kama mchumba wako ni mpenda fedha kama kila wakati anahitaji pesa kutoka kwako bila kujali unazo au hauna na wakati mwingie hata kwa mambo ambayo anaweza kuyafanya bila msaada wako wa kifedha. Kwa mfano, kila wakati atakuelezea mahitaji yake ya kifedha na kuomba umsaidie. Leo anaweza kukuomba umsaidie kulipa kodi ya nyumba, kesho anakuomba fedha ya mafuta ya gari, kesho kutwa anakuomba umnunulie simu na kadhalika. Wakati anakueleza mahitaji yake, yeye hayuko tayari kukupa chochote hata kama ana uwezo wa kifedha. Ukiona dalili hizi inabidi ujiulize mara mbili mbili. Kwa kusema haya, simaanishi kuwa usimpe chochote mchumba wako. La hasha. Unapaswa kumpa kwa upendo na kwa hiari yako na siyo kugeuzwa kuwa kitega uchumi.

Hizi ni baadhi tu ya ishara kuwa mchumba wako anaweza kuwa hana upendo wa dhati kwako na ukiona tabia hizi fikria mara mbili mbili kuendelea kuwa naye katika mahusiano.

Je, ungependa kujifunza zaidi kuhusu mada hii?

Kama unataka kuendelea kujifunza zaidi kuhusu mada hii, unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala mbalimbali zitakazokusaidia kuboresha mahusiano yako iwe katika uchumba au ndoa au mahusiano mengine katika familia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla.

Zaidi ya kujifunza kuhusu mahusiano, utapata pia makala juu ya masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kujiunga na mtandao huu, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa.

Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

1 comment / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *