Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Umewahi kusikia kuhusu jarida la Forbes? Hili ni jarida maarufu la kibiashara la Marekani ambalo huchapisha masuala ya fedha, viwanda, uwekezaji na masoko. Jarida hili ni maarufu sana duniani kwa kutoa takwimu, orodha na madaraja ya vitu kama vile orodha ya watu matajiri (mabilionea) zaidi duniani (the Word’s Billionaires).
Januari 7, 2021, gazeti la Forbes lilimtangaza Elon Musk raia wa Marekani na mzaliwa wa Afrika kusini, kuwa bilionea mpya wa dunia ambaye kwa sasa ana utajiri (net worth) wa dola za Kimarekani bilioni 219. Tangu wakati huo, Elon Musk amekuwa ndiye tajiri namba moja duniani hadi sasa na alichukua nafasi ya bilionea Jeff Bezos ambaye alikuwa ameshikilia nafasi hiyo tangu mwaka 2017.
Watu wengi walimpongeza Elon Musk kwa mafanikio hayo. Lakini wengi hawajui jinsi alivyofika hapo. Makala haya yataeleza kwa kifupi siri mojawapo ya mafaniko ya Musk na nini tunaweza kujifunza kutoka kwake na watu wengine wenye tabia kama yake.
Moja ya siri kuu ya mafanikio ya Elon Musk ni usomaji wa vitabu. Wakati akiwa shule ya msingi alikuwa akitumia muda usiopungua saa kumi kwa siku kusoma vitabu na aliwahi kusoma vitabu vyote katika maktaba mojawapo nchini mwake. Aidha, anashikilia rekodi ya kusoma encyclopedia Britannica yote yenye jumla ya kurasa 32,640 sawa na vitabu 163 vyenye wastani wa kurasa 200 kila kimoja. Vilevile, Elon Musk, ambaye amewekeza katika kampuni ya safari za anga na kampuni ya magari ya umeme, alijifunza teknolojia ya vyombo vya angani (rockets) na magari ya umeme kwa kusoma vitabu tu.
Matajiri wengi duniani ni wasomaji wa vitabu
Usomaji wa vitabu si tabia ya Elon Musk pekee yake, bali ni tabia ya watu wengi waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali za maisha. Wengi waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali za maisha hawana elimu kubwa sana ya darasani bali wana elimu kubwa waliyoipata nje ya darasa kwa kusoma vitabu. Hata nchi zenye maendeleo makubwa, watu wake ni wasomaji wa vitabu. Nitatoa mifano michache.
Usomaji wa vitabu unatajwa kuwa ni mojawapo ya sababu za maendeleo ya nchi ya Marekani na watu wake. Marekani ni moja ya nchi zenye yenye maendeleo makubwa duniani na tafiti zinaonesha kuwa, 72% ya wamarekani ni wasomaji wa vitabu na husoma kati ya vitabu 4 – 12 kwa mwaka. Takwimu hizi ni kwa kwa watu wa kawaida tu. Lakini wafanyabiashara, wawekezaji na wenye majukumu ya kiuongozi wanasoma zaidi. Takwimu zinaonesha kuwa kwa wastani, Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi husoma kati ya vitabu 4-5 kwa mwezi.
Jeff Bezos, mwanzilishi wa kampuni ya Amazon na tajiri namba tatu duniani akiwa na utajiri wa dola bilioni 143, kitu chake cha kwanza kila siku anapoamka ni kusoma kitabu. Bill Henry Gates, tajiri namba tano duniani (akiwa na utajiri wa dola bilioni 104) na aliyewahi kuwa tajiri namba moja duniani kuanzia mwaka 1995 hadi 2017 (isipokuwa kwa miaka minne tu katika kipindi hicho) husoma wastani wa kitabu kimoja kwa wiki. Warren Buffett, tajiri namba sita duniani (akiwa na utajiri wa dola bilioni 100) husoma kurasa zisizopungua 600 kwa siku (sawa na wastani wa vitabu vitatu vyenye kurasa 200 kila kimoja) na asilimia 80 ya muda wake kwa siku anautumia kusoma vitabu. Mark Zuckerberg, mwanzilishi wa mtandao wa facebook na tajiri namba 25 duniani (akiwa na utajiri wa dola bilioni 47) husoma vitabu visivyopungua viwili kwa mwezi. Bilionea mwingine, Mark Cuban, mmiliki wa timu ya mpira wa kikapu ya Marekani, Dallas Mavericks, hutumia zaidi ya saa 3 kwa siku kusoma vitabu. Taarifa hizi kuhusu nafasi ya matajiri wa dunia ni kama zilivyochapishwa katika Mtandao wa Forbes the world’s real-time billionaire leo tarehe 25 Oktoba, 2022. Mtandao huu huchapisha orodha za matajiri wa dunia kila siku.
Usomaji wa Biblia na mafanikio
Mafanikio ya kweli yanahusisha kuishi kulingana na maelekezo ya Mungu. Pamoja na mambo mengine, mafanikio ya kweli yanachangiwa na usomaji wa Neno la Mungu. Ipo mifano mingi ya watu waliofanikiwa kutokana na kusoma Neno la Mungu. Mmoja wa watu hao ni Danieli kama anavyoeleza yeye mwenyewe “Mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini” (Danieli 9:2). Danieli alifanya ya ajabu yaliyotikisa dunia ya wakati wake. Kumbe siri ya mafanikio yake ni usomaji wa vitabu!
Mtu mwingine ni mtume Paulo ambaye amefanya kazi kubwa kuliko mitume wote wa agano Jipya. Ameandika vitabu 14 kati ya vitabu 27 vya agano jipya. Naye siri ya mafanikio yake ni kusoma vitabu! Paulo alikuwa anathamini sana vitabu kama kauli yake kwa Timotheo inavyothibitisha “Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya ngozi” (2 Timotheo 4:13). Kwa kusoma sana vitabu, Paulo alikuwa anajua mambo mengi hadi baadhi ya watu wakadhania kuwa ana wazimu maana aliongea vitu vigumu na vilvuo juu ya upeo wa watu wengi kiasi kwamba watu nwengi walikuwa hawamuelewi wakiwemo wafalme. Kuna wakati Mfalme Festo aliwahi kusema ‘‘Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili. Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili” (Matendo 26:24-25).
Katika agano la Kale, Mungu alimwambia Yoshua awe msomaji wa kitabu cha Torati ili aweze kufanikiwa katika mambo yake. ‘‘Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana’’(Yoshua 1:8). Yoshua alikuwa msomaji mzuri wa vitabu, licha ya kwamba tayari Musa alikuwa amemuwekea mikono na kumjaza roho ya hekima (Kumb. 34:9). Ikiwa mtiwa mafuta wa Bwana kama Yoshua alikuwa msomaji wa vitabu, kwa nini mimi na wewe tusiwe wasomaji wa vitabu?
Kwa mifano hii michache ni dhahiri kwamba usomaji wa vitabu ni siri mojawapo ya mafanikio ya aina yoyote, yawe ya kiuchumi, kiafya, kijamii, kiroho, kimahusiano na kadhalika. Kwa bahati mbaya, watu wengi hawaoni kuwa usomaji wa vitabu ni kitu muhimu hasa katika kipindi hiki tunachoishi chenye “kelele” na usumbufu mwingi kutoka kwenye mitandao ya kijamii, simu, televisheni, radio na vyanzo vingine vya habari na taarifa. Wakati Jeff Benzos kitu chake cha kwanza kushika anapoamka ni kitabu,watu wengi wa leo kitu chao cha kwanza kushika ni simu! Ukiacha simu, watu wengi wanatumia muda mwingi kwenye televisheni, radio na mitandao ya kijamii wakifuatilia habari na matukio kuliko kusoma vitabu. Kutoona umuhimu wa kusoma vitabu ni sababu mojawapo kubwa ya matatizo na changamoto ambazo watu wengi wanazipitia kwenye maisha yao.
Ni ukweli ulio wazi na hata Biblia inaeleza kuwa hakuna kitu kipya chini ya jua. “Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua” (Mhubiri 1:9). Kila kinachotokea sasa, kilishatokea huko nyuma, lakini kinachotokea sasa kinaweza kuwa kinatokea kwa namna tofauti na kilivyotokea huko nyuma. Hata matatizo na changamoto zilizopo leo zinaweza zisiwe mpya na ni watu wengi tu wamezipitia na wapo waliozitatua na wengine ziliwashinda. Baadhi ya wale waliozitatua, waliandika sulushisho la changamoto hizo katika vitabu. Hivyo, ukisoma vitabu unaweza kupata suluhisho la changamoto yako kutoka kwa watu waliozipitia na kuzitatua. Hivyo, si kitu cha kushangaza kuwa watu wengi waliofanikiwa katika maisha ni wasomaji wa vitabu.
Je, unataka kuwa mmoja wa watu waliofanikiwa dunaiani? Basi, nakushauri uwe msomaji wa vitabu. Na wala usingoje kesho bali anza leo hii. Pamoja na vitabu vingine, tunakukaribisha ujipatie vitabu vyetu ili uweze kupata maarifa kuhusu mafanikio katika maeneo ya fedha, uwekezaji, biashara, mahusiano na mambo ya kiroho, Kwa sasa tuna vitabu vifuatavyo:
- Siri za Mafanikio ya Kifedha Katika Ndoa na Familia
- Mwonekano wa Mkristo: Kanuni zinazokubalika Kibiblia, Kijamii na Kiafya kuhusu Mavazi, Mapambo na Vipodozi
- Homilia kwa Walei: Ustadi wa Kuandaa na Kuwasilisha Mahubiri
- Ustadi wa Kuhubiri na Kufundisha Watoto
Kwa maelezo zaidi kuhusu vitabu hivi na namna ya kuvipata bonyeza hapa.