Rafiki yangu Mpendwa,
Mikopo na madeni ni sehemu ya maisha kwa watu wengi leo. Pamoja na manufaa makubwa yanayoweza kupatikana kupitia mikopo, kuna changamoto na hatari nyingi zinazotokana na mikopo.
Watu wengi wamekuwa wakiingia kwenye madeni mabaya na yanayowatesa kwa sababu tu hawajui hatari za mikopo, na hilo limekuwa kikwazo kikubwa kufikia mafanikio ya kifedha. Mbaya zaidi, kuna upotoshaji na uongo mwingi na dhana zisizo sahihi kuhusu mikopo. Hivyo, kuna haja ya kufahamu uzuri na ubaya wa mikopo ili kufaidika nayo au kuepuka hatari zitokanazo na mikopo. Hivyo, fuatana nami tunapoliangalia suala hili kwa mtazamo wa kibiblia.
Awali ya yote , ieleweke kuwa hakuna andiko katika Biblia linalosema kwamba kukopa ni dhambi au kukopesha ni dhambi. Yapo mafungu kadhaa ambayo ama moja kwa moja au isivyo moja kwa moja yanaonesha kuwa kukopa na kukopesha ni kitu kilichokuwa kinaruhusiwa tangu zamani. Mifano ya mafungu hayo ni Zaburi 112:5 linalosema “Heri atendaye fadhili na kukopesha.”
Vilevile, Biblia inasema “Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, usifanye moyo wako kuwa mgumu, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini; lakini mfumbulie mkono wako kwa kweli, umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja yake katika ahitajiayo” (Kumb.15:7, 8). Maandiko haya yanaashiria kuwa kukopesha ni jambo jema kwani kufanya hivyo ni kuonesha upendo kwa kuwasaidia wanadamu wenzako walio wahitaji.
Tangu awali, Mungu aliahidi baraka kwa watu wake ikiwa watatii sauti yake. Moja ya ahadi hizo ni kwamba watakuwa wakopeshaji na si wakopaji (Kumb. 28:12). Kwa kuwa Waisraeli kwa nyakati mbalimbali hawakuitii sauti ya Mungu na hasa baada ya kuchangamana na mataifa mengine ambapo walianza kuabudu miungu ya kigeni, hivyo hawakufaidi baraka ya kuwa wakopeshaji. Badala yake nao walianza kukopa.
Kwa kujua hatari za madeni, Mungu alitoa maelekezo kuhusu kukopeshana (Mambo ya Walawi 25:35-41, Kutoka 22:25-27, Kumb.15:1-2; Kumb. 23:19-20) kama ifuatavyo:
- Ndugu yako akiwa na matatizo msaidie, usimkopeshe,
- Ndugu yako mwenye shida unaweza kumpa kazi akufanyie na kumlipa ujira,
- Kama ni lazima kumkopesha ndugu yako, usimkopeshe kwa riba,
- Mtu wa taifa jingine unaweza kumkopesha kwa riba,
- Mtu anapokopa ni lazima alipe deni lake kwa wakati,
- Wanaodaiwa hawapaswi kunyanyaswa.
Je, Mungu anapenda tukope?
Pamoja na kwamba maandiko yanaonesha kuwa kukopa na kukopesha ni jambo linaloruhusiwa, lakini haukuwa mpango wa Mungu kuwa watu wake wawe watumwa wa madeni. Ndiyo maana katika Agano la Kale, Mungu aliweka utaratibu wa kuwatoa watu katika utumwa wa madeni kila mwaka wa saba.
Vilevile, kila baada ya mzunguko wa Sabato saba za mwaka kila aliyekuwa ameuzwa au ardhi yake ilikuwa imeuzwa ili kulipa deni aliachiwa huru au kurudishiwa ardhi yake. “Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio. Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya Bwana. Waweza kumtoza mgeni; lakini kila uwiacho kwa nduguyo mkono wako utamwachilia” (Kumb. 15:1-2). Soma pia Mambo ya Walawi 25:23-55.
Katika Agano Jipya, kuna ushahidi pia kuwa madeni haukuwa mpango wa Mungu. Katika Warumi 13:8, Paulo anashauri “Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza Sheria”. Japo anachokizungumzia Paulo ni zaidi ya kudaiwa fedha, lakini kinahusisha pia wajibu wa kulipa kila unachodaiwa na wengine.
Maandiko katika Agano la Kale na Jipya, yanaonesha wazi kuwa kudaiwa si kitu kinachofaa. Pamoja na ukweli huu, lakini uhalisia unaonesha kuwa mikopo na madeni ni sehemu ya maisha ya watu wengi. Watu wamekuwa wakiangukia katika utumwa huo kutokana na sababu mbalimbali kama vile kukopa ili kupata fedha za kukabiliana na majanga au mahitaji fulani ya msingi.
Aidha, watu wengi, wakiwemo wakristo, huingia katika madeni kwa sababu ya kukosa elimu ya msingi kuhusu usimamizi wa fedha binafsi. Wakristo kuingia katika utumwa wa madeni, haiondoi ukweli kwamba madeni ni mabaya. Wakristo wanahitaji kupata elimu itakayowasaidia kuepuka utumwa wa madeni.
Hapo ndipo kuna haja ya kupata vitabu vizuri vya elimu ya fedha ambavyo vinaeleza kwa kina suala la mikopo na madeni. Mojawapo ya vitabu hivyo ni kitabu kiitwacho “Siri za Mafanikio ya Kifedha katika Ndoa na Familia: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi za Kukabiliana na Migogoro na Changamoto za Kifedha Katika Ndoa na Familia”.
Zaidi ya kupata elimu sahihi kuhusu Mikopo na Madeni katika kitabu hiki, utajifunza mambo mengi kuhusu elimu ya fedha kwa muktadha wa kibiblia na namna unavyoweza kuitumia elimu hiyo katika kusimamia fedha zako kama mwanandoa na mwanafamilia,. Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hicho bonyeza hapa.
Makala haya yataendelea………..
Endelea kufuatilia mtandao huu ili upate mwendelezo wa makala haya. Ili usipitwe na yoyote, unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala moja kwa moja kupitia email yako kila zinazowekwa kwenye mtandao.
Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.
3 comments / Add your comment below