Rafiki yangu mpendwa,
Katika makala yaliyopita, tuligusia kidogo suala la kukopesha kwa riba. Katika makala ya leo, tutaliangalia suala hili kwa undani kidogo ili kuona kama Biblia inaruhusu kukopesha kwa riba au ala.
Kusoma makala juu ya ‘Biblia inasemaje kuhusu kukopa na kukopesha’ bonyeza hapa
Biblia imetoa miongozo bayana kuhusu kukopeshana ambapo imeeleza ni nani na katika mazingira gani unaweza kumkopesha kwa riba au bila riba. Baadhi ya mafungu ya Biblia yanayotoa mwongozo huo ni pamoja na Mambo ya Walawi 25:35-37, Kutoka 22:25, Kumbukumbu la Torati 15:1-2; 23:19-20.
Kupitia mafungu haya, tunapata miongozo mikuu miwili: Kwanza, kama ni lazima kumkopesha ndugu yako, usimkopeshe kwa riba. Pili, Mtu mgeni (wa taifa jingine) unaweza kumkopesha kwa riba. Hebu sasa fuatana nami tuweze kuchambua miongozo hii.
Tofauti kati ya mikopo ya uzalishaji na isiyo ya uzalishaji
Tangu zamani za Biblia kumekuwa na tofauti baina ya mikopo ya uzalishaji (productive loans) na mikopo isiyo ya uzalishaji (unproductive loans). Kabla hatujaendelea mbele, ni muhimu kuelewa tofauti hii maana ndiyo msingi wa sheria ya kuzuia au kuruhusu riba katika maandiko.
Mikopo ya uzalishaji ni mikopo inayochukuliwa ili kupata kianzio au mtaji wa biashara au uwekezaji. Mikopo isiyo ya uzalishaji ni mikopo inayochukuliwa ili kukidhi mahitaji (matumizi) kawaida au mahitaji maalum baada ya mtu kushindwa kuyamudu kupitia vyanzo vyake vya kawaida vya kujipatia riziki.
Kwa muktadha huu, sheria iliyokuwa inazuia kukopesha kwa riba, ilihusu mikopo isiyo ya uzalishaji tu. Hivyo, riba ilikuwa inaruhusiwa katika mikopo ya uzalishaji. Kwa muktadha huo huo, leo tunaweza kutoza riba kwa mikopo ya uzalishaji lakini si vema kutoza riba kwa mikopo isiyo ya uzalishaji. Ukisoma kisa cha talanta katika Mathayo 25:27 au Luka 19:23, utagundua kuwa Yesu mwenyewe alitoa kauli inayoashiria kuwa ni halali kuwatoza riba wakopaji.
Kwa nini Mungu alikataza riba kwenye mikopo isiyo ya uzalishaji?
Muktadha wa sheria inayozuia kutoza riba katika mafungu yaliyotajwa hapo juu ni kuzuia unyanyasaji na maumivu kwa maskini na wahitaji. Kama nilivyoeleza hapo juu, mikopo isiyo ya uzalishaji ni kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya mtu anayechukua mkopo ambayo, kwa kawaida hayawezi kusubiri. Mifano ya mahitaji hayo ni kama vile ada ya shule, matibabu, chakula na mahitaji mengine kama hayo.
Hadi mtu afikie hatua ya kukopa, maana yake hana uwezo au hana namna nyingine ya kugharamia mahitaji yake kwa wakati huo. Sababu za kukosa uwezo ni nyingi kama vile umaskini, ugonjwa, kupatwa na majanga kama vile ajali na kadhalika.
Kumtoza riba mtu asiye na uwezo wa kugharamia mahitaji yake ni sawa na kumuongezea matatizo aliyo nayo. Fikiria mtu amekosa Sh.1,000,000 kwa ajili ya matibabu na wewe ukamkopesha kwa riba ya 20% maana yake atalazimika kukulipa Sh. 1,200,000. Sasa kama alikosa Sh. 1,000,000, hiyo Sh. 1,200,000 ataitoa wapi? Badala ya kumsaidia kuondokana na shida yake, wewe unamuongezea shida zaidi!
Ili kuzuia unyanyasaji na maumivu kwa maskini na wahitaji, Mungu alikataza riba kwa mikopo isiyo ya uzalishaji na akatoa miongozo yenye lengo la kumsadia mhitaji. Baadhi ya mafungu yanayotoa miongozo hiyo ni Mambo ya Walawi 25:39-42; Kutoka 22:25-27; Kumbukumbu la Torati 15:7-11; 23:19; Mathayo 5:42 na Luka 6:35-36.
Kutoka katika mafungu haya tunapata miongozo ifuatavyo:
- Ndugu yako akiwa na matatizo msaidie, usimkopeshe. Ikiwa ni lazima umkopopeshe, usimtoze riba.
- Mtu anapokopa ni lazima alipe deni kwa wakati. Hata hivyo, asipolipa kwa wakati hapaswi kunyanyaswa.
- Ndugu yako mwenye uhitaji unaweza kumpa kazi akufanyie na umlipe ujira.
- Zaidi ya kuzuia maumivu na unyanyasaji kwa maskini na wahitaji, sheria ya kutotoza riba ililenga kuimarisha upendo wa kindugu na moyo wa kusaidia wahitaji bila kutarajia chochote kutoka kwao.
Riba kwa wageni
Biblia inaruhusu kuwatoza riba wageni. Kwa Mfano, katika Kumbukumbu la Torati 23:20, Biblia inasema “Mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki”.
Kwa muktadha wa fungu hili, wageni ni watu wa mataifa mengine, watu wasio waisraeli. Wageni wanaotajwa hapa ni wale waliokuwa wanakuja kwa shughuli za kibiashara kutoka katika mataifa mengine. Hivyo, utozaji wa riba unaozungumziwa hapa haupaswi kueleweka kama ubaguzi wa utaifa bali unapaswa utazamwe kwa jicho la kutofautisha baina ya kumkopesha maskini au mhitaji katika jamii inayokuzunguka na kumkopesha mfanyabiashara wa kimataifa.
Unapomkopesha maskini au mhitaji, unamsaidia kukabiliana na mahitaji yake lakini unapomkopesha mfanyabiashara wa kimataifa, unamsaidia kupata au kuongeza mtaji wa biashara yake ili apate faida. Kwa mazingira hayo, hakukuwa na ubaya wowote kujipatia faida kwa kumtoza riba mgeni kwa kuwa na yeye alikuwa anautumia mkopo huo kujipatia faida.
Mifano ya manyanyaso na maumivu kwa wakopaji katika Biblia
Maandiko yameeleza habari za watu walioingia katika madeni na mambo magumu waliyopitia. Mfano mmoja ni tukio la mkopeshaji kutaka kuchukua watoto wa mdeni wake katika kitabu cha 2 Wafalme sura ya 4.
Biblia inaeleza kuwa “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa” (2 Wafalme 4:1).
Yule mjane alikuwa amebakiza mafuta kidogo nyumbani na Elisha aliomba kwa Mungu yale mafuta yakaongezeka na kujaa vyombo vingi na yule mama aliyauza na kupata fedha ya kulipa deni.
Katika kitabu cha Nehemia sura ya 5, tunakutana na habari nyingine kuhusiana na namna riba ilivyokuwa inatesa watu. Sura hii inaelezea namna Nehemia alivyoshughulikia dhuluma itokanayo na riba miongoni mwa wana wa Israeli baada ya kuwa wamerudi kutoka utumwani Babeli.
Njaa na ukame vilivyokuwa vimeikumba nchi viliacha baadhi ya familia zikiwa hazina uwezo wa kulipa kodi kwa serikali ya Waajemi na hata kumudu mahitaji muhimu kama chakula. Kutokana na changamoto hiyo, Wayahudi walilazimika kuweka rehani nyumba zao, mashamba yao na mashamba yao ya mizabibu ili wapate fedha ya kulipa kodi na kumudu mahitaji yao.
Kama tulivyoona kwenye kisa cha mwnamke mjane, mojawapo ya desturi ilikuwa ni kuuza watoto ili wawe watumwa au wao wenyewe (wadaiwa) kwenda utumwani kama njia ya kulipa deni. Nehemia alighadhabika sana alipogundua kuwa Wayahudi walikuwa wakiwatoza riba na kuwanunua au kuwatumikisha Wayahudi wenzao kama watumwa.
Japokuwa, desturi hiyo ilikuwa halali kisheria, lakini haikuwa halali kimaadili kwa maana ilikuwa ya kionevu na kinyanyasaji. Kwa sababu hiyo, Nehemia aliipinga na kuwataka matajiri warejeshe kila kitu walichopokonya kutoka kwa ndugu zao walio maskini. Kama ilivyoelezwa awali, kukopesha ndugu yako kuliruhusiwa na sheria, lakini kutoza riba hakukuruhusiwa bila kujali kama riba hiyo ni ndogo kiasi gani.
Wakati wa Nehemia, wakopaji walitakiwa kulipa riba ya asilimia 12 kwa mwaka. Riba hii ilikuwa ni ndogo ikilinganishwa na ile iliyotozwa na mataifa ya jirani. Kwa mfano, maandishi ya Wamesopotamia tangu karne ya saba yanaonesha riba ya asilimia 50 ilitozwa na wakopeshaji wa fedha na riba ya asilimia 100 ilitozwa na wakopeshaji wa nafaka kila mwaka.
Pamoja na riba hii kuwa ni ndogo lakini ilikuwa haikubaliki kulingana na Neno la Mungu. Kwa kuzingatia hilo, Nehemia alikasirika sana na akaamua kulipinga suala hili kwa uthabiti wa hali ya juu na kuwataka wakopeshaji kuacha kabisa kufanya hivyo. Baada ya Nehemia kuingilia kati, wakopeshaji waliacha kutoza riba na wakawarudishia riba walikuwa wametoza.
Kwa kuwa Neno la Mungu limetoa miongozo bayana kuhusu kukopeshana, hatuna budi kuizingatia hata kama sheria za nchi na destruri za jamii tunayoishi ziko tofauti na miongozo hiyo. Nehemia hakuacha kushughulikia malalamiko ya watu kuchukuliwa utumwani eti kwa sababu yalikuwa hayavunji sheria au kwa kuwa yalikuwa yanakubalika kijamii kulingana na desturi za nchi. Katika wakati wa shida za kiuchumi ziliyokuwa zinawakabili, ilikuwa ni wajibu wa watu kusaidiana. Lakini wao walitumia hali hiyo kujitajirisha bila kujali kuwa kwa kufanya hivyo waliwaumiza ndugu zao. Ilibidi Mungu awaagize manabii kuzungumza dhidi ya maovu na vurugu iliyotendwa dhidi ya maskini. Nasi yatupasa kufanya vivyo hivyo leo.
Kama unataka kujifunza zaidi kuhusu somo hili unawe\a kujipatia kitabu kiitwacho “Siri za Mafanikio ya Kifedha katika Ndoa na Familia: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi na Kukabiliana na Migogoro na Changamoto za Kifedha Katika Ndoa na Familia”. Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hicho bonyeza hapa.
Makala haya yataendelea………………..
Endelea kufuatilia mtandao huu ili upate mwendelezo wa makala haya. Unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala moja kwa moja kupitia email yako kila zinazowekwa kwenye mtandao.
Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.
1 comment / Add your comment below