Rafiki yangu mpendwa,
Mwandishi maarufu wa karne ya 19 na 20 wa vitabu vya kikristo na machapisho mengine aitwaye Ellen G. White, katika kitabu chake kiitwacho Counsels on Stewardship, uk. 272 ameandika “Ni lazima kuwepo na zingatio makini kuhusu uchumi, la sivyo deni kubwa litapatikana. Dumu katika mipaka. Epuka upatikanaji wa deni kama vile ambavyo ungeliepuka ugonjwa wa ukoma”.
Katika zama hizi, ugonjwa wa ukoma si tishio ukilinganisha na magonjwa mengine kama vile UKIMWI, saratani, kisukari na UVIKO-19. Lakini kwa miaka ya nyuma, ukoma ulikuwa moja ya magonjwa mabaya. Hata katika nyakati za Biblia, wagonjwa wa ukoma walitengwa na jamii hadi hapo makuhani wakipojiridhisha kuwa wamepona kabisa. Katika muktadha huo, Ellen White, anawaasa wasomaji wake kuogopa deni kama ukoma. Angekuwa anaandika leo, huenda angetaja magonjwa mengine ambayo ni tishio kwa sasa.
Kwa kulinganisha madeni na ugonjwa hatari kama ukoma, ni dhahiri kwamba madeni ni hatari. Pamoja na manufaa ambayo tunaweza kuyapata kwa kuchukua mikopo, lakini tunapaswa kuwa makini ili madeni yatokanayo na mikopo yasigeuke kuwa hatari kama ukoma.
Kujifunza zaidi kuhusu mikopo soma hapa: Biblia Inasemaje Kuhusu Kukopa na Kukopesha?
Soma pia: Biblia Inasemaje Kuhusu Kukopesha kwa Riba?
Katika makala haya, nitakushirikisha baadhi tu ya sababu kwa nini, unapaswa kuepuka madeni kama ukoma. Baadhi ya sababu hizo ni kama ifuatavyo:
- Madeni ni Utumwa
Neno la Mungu linaeleza “Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye”(Mithali 22:7). Simulizi mbalimbali za Biblia zinaeleza namna madeni yalivyokuwa yanasababisha watu kwenda utumwani enzi za Agano la Kale.
Kimsingi hali haijabadilika. Madeni bado ni utumwa hata leo. Tofauti tu ni kwamba, utumwa unaotajwa katika biblia ni utumwa wa kimwili lakini utumwa wa leo ni utumwa wa hofu na kukosa uhuru kwa sababu ya kudaiwa. Madeni ni utumwa kwa sababu zifuatazo:
- Ukiwa na deni unakosa uhuru wa kutumia fedha yako. Ukishakuwa na deni ina maana sehemu ya kipato chako, kinakwenda kulipa deni, hivyo huwezi kukitumia kipato hcho kama unavyotaka wewe. Kwa mfano, kama mshahara wako ni Sh. 1,000,000 na ukaingia kwenye mkopo na marejesho yake ni Sh. 400,000 kwa mwezi, hapo kipato chako kinashuka na kuwa Sh. 600,000 tu na siyo sh. 1,000,000. Ni dhahiri, hapa hauna uhuru wa kutumia fedha yako yote kwa kipindi chote cha kulipa mkopo.
- Anayekudai anakuwa ni tishio kwako na unakuwa na hofu naye kwa sababu anaweza kuchukua hatua yoyote mbaya dhidi yako ikiwa pamoja na kukudhalilisha.
- Unakuwa unawafanyia wengine kazi. Kwa mfano, Ukikopa shilingi milioni moja lakini unakuja kulipa hiyo milioni moja na riba juu. Kwa kulipa riba unakuwa umemfanyia kazi na kumzalishia yule aliyekukopesha.
- Unaadhibiwa kwa kukopa. Unaweza kujifariji kuwa mkopo umekusaidia katika kufanikisha mambo yako, lakini ukweli ni kwamba kwa kulipa riba ni dhahiri kuwa umeadhibiwa. Riba ndiyo adhabu ya kukopa. Kwa mfano, unakopa Sh.1,000,000 unalipa Sh.1,200,000. Hiyo sh. 200,000 ya ziada (riba) ndiyo adhabu ya kukopa.
2. Kama umeweka mali yako kama dhamana ya mkopo na ukashindwa kulipa mkopo, unaweza kupoteza mali hiyo. Hii inaweza kukuingiza katika umaskini au hali ngumu ya maisha. Vipo visa vingi vya watu walioathirika vibaya kiuchumi baada ya raslimali zao kama vile nyumba na ardhi kuuuzwa au kuchukuliwa ili kulipa deni.
3. Madeni yanaweza kusababisha migogoro ya ndoa hasa pale mwanandoa mmoja anapochukua mkopo bila kumshirikisha mwenzi wake na akashindwa kulipa mkopo huo. Ndoa nyingi zimevunjika kwa sababu ya migogoro itokanayo na madeni.
4. Ukiwa na madeni na ukawa msumbufu kulipa unajishushia heshima au hadhi yako katika jamii. Kama wewe ni Mkristo unaweza kusababisha jina la Mungu litukanwe na utakosa uhuru wa kutangaza Injili kwa watu wanaokufahamu.
5. Ukiwa na madeni na ukashindwa kulipa, unaweza kupata msongo wa mawazo. Kwa sababu ya madeni, baadhi ya watu wamechukua maamuzi mabaya kama vile kujinyonga, kukimbia deni na hivyo kutelekeza familia iliyokuwa inawategemea na kuwafanya wanafamilia kuishi maisha magumu.
6. Madeni yanaweza kusababisha kuvunjika kwa uhusiano baina ya mkopaji na mkopeshaji. Kwa mfano, kama umemkopesha ndugu au rafiki yako asipokulipa uhusiano wenu unaweza kugeuka uadui.
7. Madeni yanaweza kukusababishia kuingia katika dhambi zifuatazo:
- Kusema Uongo: Unaweza kujaribiwa kusema uongo ili kumfanya anayekudai asikusumbue. Kwa mfano, unaweza kudanganya kuwa umeshindwa kulipa kwa sababu ulipata matatizo kama vile kuuguliwa au kuugua wewe mwenyewe, kufiwa mtu wa karibu, kupata hasara kwenye biashara, kuibiwa na kadhalika ilhali siyo kweli.
- Kutorudisha zaka na sadaka: Utoaji wa zaka na sadaka ni sehemu ya maisha ya Mkristo na ni kipimo cha utii na shukurani kwa Mungu. Hata hivyo, katika kipindi unacholipa mkopo, kipato chako kinapungua na hivyo unaweza kuingia katika jaribu la kutokurudisha zaka na sadaka kwa hoja kwamba kipato kinachobaki hakikidhi mahitaji yako muhimu kama ilivyokuwa kabla ya kuchukua mkopo. Ili uendelee kuishi maisha ya hadhi ile ile kabla ya mkopo unaweza ukaamua kutorudisha zaka na kutotoa sadaka.
- Kufanya kazi siku saba: Katika jitihada za kulipa mkopo wako kwa uaminifu, wakati mwingine itabidi ufanye kazi zaidi ili kuongeza kipato. Unaweza kufanya kazi siku saba kwa wiki na kutopumzika siku ya saba kwa kudhani kuwa kupumzika siku ya hiyo ni kupunguza kipato. Kwa kutopumzika siku ya Saba unakuwa unavunja amri ya nne ya Mungu (Kutoka 20:8-11).
Ungependa kujifunza zaidi juu ya mada hii?
Pamoja na mikopo kuwa na uwezekano wa kutuingiza katika madeni, lakini uhalisia unaonesha kuwa mikopo ni sehemu ya maisha ya watu wengi na wapo walionufaika na mikopo na wakapata mafanikio makubwa ya kiuchumi.
Kinachowafanya wengi waingie katika hatari za madeni ni kukosa elimu sahihi juu ya usimamizi wa fedha binafsi ikiwa pamoja na elimu sahihi kuhusu mikopo. Hapo ndipo kuna haja ya kupata vitabu vizuri vya elimu ya fedha ambavyo vinaeleza kwa kina suala la mikopo na madeni ili uweze kunufaika na mikopo na kuepuka hatari zitokanazo na madeni.
Mojawapo ya vitabu hivyo ni kitabu kiitwacho “SIRI ZA MAFANIKIO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi na Kukabiliana na Migogoro na Changamoto na Kifedha Katika Ndoa na Familia”.
Zaidi ya kupata elimu sahihi kuhusu Mikopo na Madeni, katika kitabu hiki, utajifunza mambo mengi kuhusu elimu ya fedha kwa muktadha wa kibiblia na namna unavyoweza kuitumia elimu hiyo katika kusimamia fedha zako kama mwanandoa na mwanafamilia. Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hicho bonyeza hapa.
Makala haya yataendelea………..
Endelea kufuatilia mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili upate mwendelezo wa makala haya.
Ili uweze kupata makala moja kwa moja kupitia email yako kila zinazowekwa kwenye mtandao huu, unaweza kujiunga na mtandao huu kwa kujaza fomu iliyopo hapa chini.
Kitabu kiko vizuri