Rafiki yangu Mpendwa,
Pamoja na ukweli kwamba watu wengi wanateswa na madeni yatokanayo na mikopo lakini wapo watu ambao mikopo imewaleta mafanikio makubwa. Sasa unaweza kujiuliza, kwa nini baadhi ya watu wanufaike na mikopo wakati wengine iwatese?
Sababu ya tofauti hii iko katika aina ya mkopo ambao mtu anauchukua. Mikopo inayowatesa watu wengi ni mikopo mibaya wakati ile inayowanufaisha ni mikopo mizuri. Kwa kujua tu tofauti baina ya mikopo mizuri na mibaya, unaweza kuikwepa mikopo mibaya na kuchukua mikopo mizuri tu. Ili uweze kuelewa tofauti ya mikopo mibaya na mizuri, fuatana nami katika makala haya.
Kujua hatari za madeni bonyeza: Hizi Ndizo Sababu Kwa nini Unapaswa Kuogopa Madeni kama Ukoma
Mikopo Mizuri ni Mikopo ya Aina Gani?
Mikopo mizuri ni aina ya mkopo ambayo marejesho yake hayatoki mfukoni mwako. Yaani, wewe unachukua mkopo lakini hulipi wewe moja kwa moja ila unaulipa kwa kutumia fedha za watu wengine.
Kwa jina jingine, mikopo hii, inaitwa mikopo ya uzalishaji (productive loans). Mkopo huu unakufanya utengeneze faida na unaweza kuulipa pamoja na riba na ukabakiwa na faida. Mtu anapochukua aina hii ya mkopo anautumia kuzalisha zaidi.
Kwa mfano, kama umekopa fedha benki kwa ajili ya mtaji wa biashara na marejesho yake ni Sh.500,000 kwa mwezi wakati faida yako kutoka kwenye biashara hiyo ni Sh. 700,000 kwa mwezi.
Huu ni mkopo mzuri kwa sababu haulipi marejesho kutoka mfukoni kwako badala yake unalipa marejesho hayo kutoka kwa watu wengine, yaani unatumia faida kutoka kwenye biashara hiyo kulipa mkopo. Hii ni fedha ya watu wengine kwa sababu haitoki kwako bali ni fedha uliyoipata kutoka kwa watu wengine.
Watu huchukua mikopo mizuri kwa ajili ya kuongeza mtaji ili kupanua biashara. Watu hawa ni wale wanaoendesha biashara zenye faida tayari na wanapochukua mkopo wanakuwa wameshapiga hesabu vizuri na kujiridhisha kuwa hawatalipa mkopo kwa fedha zao bali za watu wengine. Tofauti na hapo, huo ni kopo mbaya na unapaswa kuuepuka kama ukoma.
Mikopo Mibaya ni Mikopo ya Aina Gani?
Mikopo mibaya ni aina ya mikopo ambayo mtu analipa yeye mwenyewe kutokana na kipato chake na hakuna namna yoyote anazalisha kile alichokopa ili kupata faida. Kwa jina jingine, mikopo hii inaitwa mikopo isiyo ya uzalishaji (non-productive loans).
Hii ni mikopo mibaya kwa sababu mtu anaishia kulipa fedha nyingi kuliko ambazo amekopa. Katika hali ya kawaida, mikopo ya aina hii tunapaswa kuiepuka kabisa. Kwa bahati mbaya, mikopo ya aina hii ndiyo mikopo mingi kuliko mikopo mizuri.
Mfano wa mkopo mbaya, ni mwajiriwa kuchukua mkopo na kununua gari ya kutembelea ambapo analipa mkopo moja kwa moja kupitia mshahara. Huu unakuwa mkopo mbaya kwa sababu, ile gari haizalishi chochote kinachosaidia kulipa mkopo. Hata kama gari hiyo ni ya biashara, ili uweze kuwa mkopo mzuri ni lazima faida inayotokana na gari hiyo iwe kubwa kuliko marejesho ya mkopo huo. Kama faida itakuwa ndogo kuliko marejesho, huo utakuwa ni mkopo mbaya.
Mifano mingine ya mikopo mibaya ni mikopo kwa ajili ya kununua chakula, kulipa ada ya shule, kulipa kodi za nyumba, kununua mavazi, kununua samani (furniture), kufanya sherehe na kujenga nyumba ya kuishi.
Kuna vitu vingi huwa tunavifanya kwa fedha ya mkopo tukidhani kwa kufanya vitu hivyo basi mikopo tuliyochukua ni mikopo mizuri lakini kiuhalisia ni mikopo mibaya. Kwa mfano, watu wengi huwa wanachukua mikopo ili kujenga nyumba ya kuishi wakiamini kuwa ni mkopo mzuri kwa kuwa nyumba itakuwa ni yao na hivyo wataacha kupanga na hivyo kutolipa kodi ya nyumba.
Hata hivyo, ukipiga hesabu, gharama huwa bado ziko nje ya uwezo wao kwa kipindi hicho na kwa kuwa nyumba haizalishi chochote, basi watu hao huishia kulipa mkopo kwa hela yao wenyewe tena kwa miaka mingi. Endelea kufuatilia mtandao huu ili ujue namna unavyoweza kumudu mahitaji yako bila kuingia katika mikopo.
Eneo hili la madeni limekuwa likiwatesa wengi, na kuna mambo mengi sana ya kushangaza na kusikitisha katika biashara ya kukopesha. Nimewahi kuongea na mmoja wa watu wanaofanya biashara ya kukopesha. Kwa maelezo yake, wateja wazuri wa biashara yake ni waajiriwa ambao wana kipato cha uhakika kila mwezi. Watu hao wanakopa kwa sababu hata ambazo hazipaswi mtu akope.
Unakuta mtu anakopa kwa sababu ana harusi, au anakopa alipie watoto ada ya shule, au anakopa alipe kodi ya nyumba. Ni jambo linalowaumiza wengi sana, kwa sababu wanarudisha mkopo huo na riba, wakati hakuna chochote wanachozalisha!
Hata wale wanaochukua mikopo mizuri, baadhi yao huibadilishia matumizi na kuitumia kwa mambo mengine na hivyo mikopo hiyo hugeuka kuwa mikopo mibaya. Ripoti ya utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) 2020/2021 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watu wanaokopa mikopo nchini wanaitumia kwa mambo binafsi yasiyorudisha fedha hizo.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Januari 18, 2023 jijini Dar es Salaam imeonyesha asilimia 31.8 ya wanaochukua mikopo wanazitumia kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani, asilimia 12.4 kwa ajili ya matibabu, asilimia 13.1 kwa ajili ya ada za shule na asilimia 1.1 kwa ajili ya kufanyia sherehe.
Vilevile, ripoti hiyo inasema asilimia 11.7 wanatumia fedha hizo kwa ajili ya kulipa kodi ya nyumba au makazi na asilimia 11 kwa matumizi mengine ya nyumbani ambayo hayakufafanuliwa. Kwa kuwa mikopo hii haitumiki katika uzalishaji, mikopo hii ni mikopo mibaya.
Wakopaji wachache waliosalia ndio wanatumia fedha za mikopo kwa masuala ambayo yamekusudiwa yanayoweza kuzalisha na kupata fedha za kulipa mkopo, kama vile asilimia 26.4 (biashara), kununua vifaa vya kilimo (asilimia 0.5), asilimia 8.5 (pembejeo) na asilimia 1.9 kununua ardhi ambayo hata hivyo inaweza kuwa ya biashara au shughuli nyinginezo.
Ripoti hiyo imetoka kipindi ambacho kuna taarifa za wakopaji wengi kushindwa kurejesha mikopo itolewayo na halmashauri mbalimbali nchini na kuilazimisha Serikali kukuna kichwa kutafuta njia mbadala ya utoaji wake. Vilevile, kumekuwa na taarifa mbalimbali za mikopo yenye riba kubwa inayotolewa kwa wananchi hasa watumishi wa Serikali ambayo inawashinda kurejesha. Mikopo hiyo imepewa majina mengi kama vile mikopo umiza, mikopo kausha damu na kadhalika.
Hali hiyo inadhihirisha kuwa kuna umuhimu wa kuwa na elimu sahihi kuhusu mikopo. Endelea kufuatilia mfulululizo wa makala haya kuhusu mikopo na madeni ili uweze kupata elimu sahihi iyakayokuwezesha kunufaika na mikopo badala ya kuteswa na madeni yatokanayo na mikopo.
Kupata elimu zaidi kuhusu mikopo na madeni, unaweza kupata kitabu kiitwacho “SIRI ZA MAFANIKIO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi na Kukabiliana na Migogoro na Changamoto na Kifedha Katika Ndoa na Familia”.
Katika kitabu hiki utapata elimu sahihi kuhusu Mikopo na Madeni na pia utajifunza mambo mengi kuhusu elimu ya fedha na namna unavyoweza kuitumia elimu hiyo katika kusimamia fedha zako kama mwanandoa na mwanafamilia. Kwa maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki bonyeza hapa.
Makala haya yataendelea………..
Endelea kufuatilia mtandao huu ili upate mwendelezo wa makala haya. Ili usipitwe na makala yoyote, unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala moja kwa moja kupitia email yako kila yanapowekwa kwenye mtandao.
Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.
1 comment / Add your comment below