Rafiki yangu mpendwa,
Karibu tena katika mwendelezo wa makala kuhusu mikopo na madeni. Katika makala ya nyuma nimekuwa nikikushirikisha mambo kadhaa kuhusu mada hii.
Pamoja na mambo mengine, tumejifunza kuwa hakuna andiko lolote katika Biblia linalosema kwamba kukopa ni dhambi au kukopesha ni dhambi na kwamba yapo mafungu kadhaa ambayo ama moja kwa moja au isivyo moja kwa moja yanaonesha kuwa kukopa na kukopesha ni kitu kilichokuwa kinaruhusiwa tangu zamani.
Pamoja na kwamba maandiko yanaonesha kuwa kukopa na kukopesha ni jambo linaloruhusiwa, lakini haukuwa mpango wa Mungu kuwa watu wake wawe watumwa wa madeni. Ndiyo maana katika Agano la Kale, Mungu aliweka utaratibu wa kuwatoa watu katika utumwa wa madeni kila mwaka wa saba. Katika utaratibu huo, kila aliyekuwa ameuzwa au ardhi yake ilikuwa imeuzwa ili kulipa deni aliachiwa huru au kurudishiwa ardhi yake.
Katika Agano Jipya, Paulo anashauri “Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza Sheria” (Warumi 13:8). Japo anachokizungumzia Paulo ni zaidi ya kudaiwa fedha, lakini kinahusisha pia wajibu wa kulipa kila unachodaiwa na wengine.
Maandiko katika Agano la Kale na Jipya, yanaonesha wazi kuwa kudaiwa si kitu kinachofaa. Katika makala ya nyuma nilikushirikisha sababu kadhaa kwa nini unapaswa kuogopa deni kama ukoma na pia nikakushirikisha kigezo pekee cha kuangalia ikiwa utahitaji kuingia katika mkopo.
Soma : Hizi Ndizo Sababu Kwa Nini Unapaswa Kuogopa Madeni Kama Ukoma
Lengo la kukushirikisha yote hayo ni ili uweze kupata maarifa yatakayokuwezesha kuepuka mikopo mibaya na ikiwa ni lazima uingie kwenye mikopo basi ujue ni mkopo upi unaweza kuchukua ili uweze kunufaika nao.
Soma: Kama Unataka Usiteseke na Madeni, Fahamu Tofauti Kati ya Mikopo Mizuri na Mikopo Mibaya
Leo nitakushirikisha njia za kuepukana na mikopo, hasa mkopo mibaya ambayo imekuwa ikiwaingiza wengi kwenye changamoto nyingi. Karibu ufuatane nami.
Njia pekee ya kukuwezesha kuepuka kungia katika madeni, ni kujijengea nidhamu kali ya fedha. Unaweza kujenga nidhamu kwa kufanya mambo ambayo hayatakuweka katika mazingira ya kuhitaji mkopo mbaya. Baadhi ya mambo hayo ni kama ifuatavyo:
- Kuishi kulingana na kipato chako. Hakikisha matumizi yako hayazidi mapato yako. Ili uweze kufanikiwa katika hili, ni muhimu uwe na utaratibu wa kudumu wa kupanga bajeti kabla ya kutumia fedha yoyote na matumizi yako yote yaongozwe na bajeti hiyo. Iwe mwiko kwako kutumia fedha bila bajeti au kutumia fedha zaidi ya bajeti yako.
- Uwe na utaratibu wa kudumu wa kujiwekea akiba kwa ajili ya dharura na uwekezaji. Wakati wowote katika maisha yako, uwe na akiba ya fedha ya kukutosha kwa kipindi kati ya miezi mitatu hadi sita ya mbele. Yaani, ikiwa kutatokea changamoto yoyote ya kifedha na ukawa huingizi fedha yoyote, uweze kuishi kwa akiba yako kwa muda wa kati ya miezi mitatu hadi sita wakati unajipanga kukabiliana na hali hiyo. Kwa kufanya hivyo, utaweza kuepuka kuingia kwenye mikopo katika kipindi hicho.Kama unajua baada ya muda fulani utakuwa na mahitaji makubwa ya fedha, jiandae mapema kutafuta fedha hiyo badala ya kusubiri muda wa ufike ndipo uanze kuhangaika. Kwa mfano, ada za shule na kodi za nyumba zinajulikana na siyo kitu cha dharura hivyo unapaswa kujiandaa mapema kugharamia matumizi haya. Mara tu unapolipa gharama hizi, anza kujipanga tena kwa malipo yajayo. Kwa mfano, kama unalipa kodi kila baada ya miezi sita, ukishalipa kodi, anza mara moja kujiandaa kulipa kodi nyingine. Njia moja wapo ya kujiandaa inaweza kuwa kududunduliza fedha kidogo kidogo kila mwezi.
- Usinunue kitu ambacho huwezi kukimudu. Kama kuna kitu umekipenda, lakini kwa uwezo wako wa kifedha huwezi kukimudu basi achana nacho kabisa. Kitu pekee ambacho huwezi kuacha kununua ni chakula au dawa kama unaumwa lakini vingine vyote unaweza kuviacha na maisha yakaendelea. Huwezi kufa eti tu kwa sababu umevaa nguo ya zamani baada ya kushindwa kununua nguo mpya, au umeacha kukopa nguo japo muuzaji amekupa nafasi ya mkopo. Kulipa gharama ambazo huzimudu ni tiketi ya kubaki kwenye madeni na umaskini.
- Usikope kwa ajili ya kugharamia au kununua vitu visivyozalisha. Ukifanya kosa hilo, utakuwa umechagua kubaki kwenye umaskini. Mifano ya mambo hayo ni pamoja na sherehe ya aina yoyote, gari ya kutembelea, nyumba ya kuishi na matumizi mengine madogo madogo kama vitu vya ndani. Hivi ni vitu ambavyo unapaswa kuvigharamia kwa fedha yako mwenyewe na siyo mkopo. Kama huwezi kununua vitu hivyo kwa sasa, weka akiba na ukipata fedha ya kutosha ndipo ununue au utumie, isipotosha basi achana na matumizi hayo, na badala yake kazana kujijengea kipato zaidi.
- Usichukue mkopo na kuuweka kwenye biashara ambayo haizalishi faida utakayoweza kuitumia kulipia gharama ya mkopo na wewe ukabaki na faida. Hivyo, kamwe usiingie kwenye mkopo kabla ya kukaa chini na kufanya mahesabu yako vizuri ili uone kama mkopo huo utakulipa au utakuingiza kwenye changamoto.
- Ili kuepukana na athari zitokanazo na majanga kama vile ajali, magonjwa na mambo mengine kama hayo, angalia uwezekano wa kukata bima za aina mbalimbali kama vile bima ya mali zako hasa zenye thamani kubwa, bima ya afya na bima zingine. Hapa utajiepusha na uwezekano wa kuingia kwenye mikopo ili uweze kukabiliana na majanga yanayoweza kukupata.
Naomba niishie hapa kwa leo, lakini nikukumbushe tu kuwa kama bado hujapata nakala ya kitabu cha “Siri za Mafanikio ya Kifedha katika Ndoa na Familia: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi na Kukabiliana na Migogoro na Changamoto za Kifedha Katika Ndoa na Familia”, basi fanya utaratibu ukipate.
Katika kitabu hiki, utajifunza mambo mengi kuhusu elimu ya fedha kwa muktadha wa kibiblia na namna unavyoweza kuitumia elimu hiyo katika kusimamia fedha zako kama mwanandoa na mwanafamilia. Ndani ya kitabu hiki, suala la mikopo na madeni limechambuliwa kwa kina. Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki na namna ya kukipata bonyeza hapa.
Makala haya yataendelea………..
Endelea kufuatilia mtandao huu ili upate mwendelezo wa makala haya. Ili usipitwe na yoyote, unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala moja kwa moja kupitia e-mail yako kila zinazowekwa kwenye mtandao.
Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini au bonyeza hapa
1 comment / Add your comment below