Usiponielewa leo,Utanielewa Utakapotapeliwa

Rafiki yangu mpendwa,

Mwanzoni mwa mwezi huu, zilisambaa habari katika mitandao ya kijamii, magazeti, redio na televisheni kuhusu watu wapatao 300 kudai kutapeliwa na kampuni ya Bestway Capital Management (BCM) ya jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa watu waliodai kutapeliwa na kampuni hiyo, Bw. Charles Kapongo ambaye ni mkazi wa jiji Dar es salaam alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kuwa yeye na wenzake zaidi ya 300 waliwekeza mamilioni ya fedha katika kampuni hiyo ambapo  waliahidiwa kupewa faida ya asilimia sita kila mwezi lakini walipewa faida ya miezi minane tu na baada ya hapo hawakupewa tena.

Wakati Bw. Kapongo anaongea, ilikuwa zaidi ya mwaka hajapewa tena faida hiyo na wala alikuwa hajui hatima ya fedha zake alizoweka kama mtaji. “Kiingilio cha uwekezaji katika kampuni hiyo ni Shilingi milioni 23 na kuna watu wameweka hadi zaidi ya Sh. Bilioni moja, kilio ni kikubwa mimi na wastaafu wenzangu tumejaribu kutafuta suluhu bila mafanikio kwa kuwa Mkurugenzi sasa hivi hatumpati kwa simu taarifa zilizopo ni kuwa amekimbilia Dubai,” alidai Bw. Kapongo katika mahojiano na Gazeti la Mwananchi la tarehe 2 Aprili, 2023.

Gazeti la Mwananchi lilifanya jitihada ya kumtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Bw. Steven Ndaula na kufanya naye mahojiano ambapo alisema yeye kama mkuu wa kampuni hiyo, amekuwa akiwasiliana na wateja mara kwa mara kwa barua na mikutano tangu kampuni yake ianze kukumbwa na mdororo na kwa mujibu wa taarifa yake, kampuni inapambana kuona namna inavyoweza kuwalipa wawekezaji wake ndani ya miaka mitatu kuanzia sasa.

Rafiki yangu mpendwa, sitaki kuihukumu kampuni ya BCM, lakini majibu ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo yanaibua maswali mengi zaidi kuliko majibu. Eti wawekezaji watalipwa ndani ya miaka mitatu! Kama makubaliano yalikuwa kulipwa kila mwezi, sasa nini kimetokea na kusababisha utaratibu huo ubadilikeke? Baada ya utaratibu kubadilika kwa nini wawekezaji hawakupewa taarifa ya mabadiliko hayo? Kwa nini Mkurugenzi hapatikani kwa simu? Anaogopa nini? Mkurugenzi anadai amekuwa akiwasiliana na wawekezaji lakini wawekezaji wanadai hawana mawasiliano hayo, nani mkweli? Kwa kifupi, kuna kila dalili kwamba wawekezaji wa kampuni ya BCM “wamepigwa”.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio mengi ya watu kuwekeza fedha nyingi katika uwezekezaji wenye utata kwa matarajio ya kupata faida kubwa tena ya chapuchapu lakini wengi wamejikuta “wakipigwa”. Miaka kadhaa iliyopita wananchi wengi walipigwa baada ya kuwekeza katika kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), maarufu kupanda mbegu na kuvuna. Kampuni hiyo ilikuwa inakusanya fedha kutoka kwa wananchi na kuwambia kuwa fedha hiyo ni mbegu na baada ya muda wangevuna fedha nyingi. Mwanzoni watu wengi walivuna kweli lakini baadaye ilibainika kuwa kampuni hiyo haikuwa na leseni kutoka benki kuu ya Tanzania na kwamba haikuwa inafanya shughuli za uwekezaji bali ilikuwa ni kampuni ya upatu na hivyo shughuli zake zilifungwa na serikali na wananchi wakapoteza fedha zao.

Inashangaza kwamba pamoja na matukio kama hayo kujirudia lakini wananchi hawashtuki bali wanaendelea kuingia kichwa kichwa na matokeo yake “wanapigwa”. Nina hakika, akitokea mtu au kampuni nyingine ya aina kama DECI na BCM, watu wengi watawekeza fedha zao katika kampuni hiyo. Huenda hata wewe unayesoma makala haya ni mmoja wa watu “waliopigwa” kupitia uwekezaji wa aina hii na kama si mmoja wao inawezekana uko tayari kuingia katika uwekezaji wa aina hiyo.

Utapeli wa aina hii si kitu kipya bali upo tangu enzi na enzi. Historia inaonesha kuwa miaka mingi iliyopita ilikuwepo dhana inayoitwa Alchemy, ambapo watu waliamini kuwa ipo namna unaweza kugeuza madini ya risasi (Lead) kuwa dhahabu. Watu wengi  walidanganyika na hali hiyo na kutafuta watu wa kubadili risasi kuwa dhahabu ili kupata utajiri. Lakini hakuna mtu aliyeweza aliyethibitika kufanya hilo, lakini bado watu waliendelea kuamini ipo namna na waliingia gharama kutafuta namna hiyo lakini hawakufanikiwa. Haya ndiyo yanayotokea sasa.

Rafiki yangu mpendwa, hakuna njia ya haraka na ya mkato ya kujipatia fedha na utajiri bila ya kufanya kazi. Hiyo haipo. Kazi ndiyo njia halali iliyowekwa na Mungu ya kujipatia fedha. Pamoja na ukweli kwamba hakuna namna mtu anaweza kupata fedha ya haraka kwa njia ya mkato bila kufanya kazi, bado watu wanaamini ipo njia ya kufanya hivyo. 

Baada ya Mungu kumuumba mwanadamu alimtwaa na kumweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza (Mwanzo 2:15). Kwa Adamu na Hawa, kulima na kutunza bustani ilikuwa ndiyo kazi yao ya kujipatia riziki. Kwa leo, zaidi ya kilimo, kuna kazi nyingine nyingi ambazo watu wanafanya ili kujipatia riziki. Si mpango wa Mungu kujipatia riziki bila kufanya kazi. Kwa kuelewa ukweli huu, hao “waliopigwa” kupitia DECI, BCM na upatu mwingine walipaswa kujiuliza: hivi, nimefanya kazi gani hadi DECI au BCM wanipatie fedha? Bila shaka jibu lao lingekuwa sijafanya kazi yoyote. Kwa jibu hili, wasingepoteza muda na fedha zako kujiunga na uwekezaji wa aina hiyo.

Narudia tena, hakuna njia ya mkato ya kupata fedha bila kufanya kazi. Haipo kabisa. Na kama ingekuwepo, ni watu wachache sana wangekuambia kuhusu njia hiyo, bali wangekuwa ‘busy’ kupata utajiri kupitia njia hiyo kabla wengi hawajaijua. Ikitokea mtu anakupa njia ya haraka na ya mkato ya kupata fedha isiyohusisha kazi, shtuka, anataka kukutapeli. Wakati mwingine anayekutapeli anajua, au hajui, kwa sababu na yeye pia ametapeliwa. Kama hutaki kutapeliwa, kaa mbali na michezo au mifumo yoyote unayoambiwa utapata fedha ya haraka bila ya kufanya kazi. Huenda hutanisikiliza na wala hutanielewa katika hili, kwa kuamini ipo siri sijaijua na sitakulaumu kwa hilo maana hutakuwa wa kwanza kuwa na mtazamo huo, lakini utanielewa vizuri ukishatapeliwa na kupotezewa muda wako.

Rafiki yangu mpendwa, si lazima ujifunze kutokana na makosa kama kuna uwekezekano wa kujifunza kutoka kwenye maarifa. Njia za kujipatia maarifa ni nyingi, mojawapo ni kusoma vitabu.

Kama unataka kupata mafanikio ya kifedha katika ndoa au familia yako na katika maisha yako binafsi, basi jipatie kitabu kinachoitwa Siri za Mafanikio ya kifedha Katika Ndoa na Familia. Kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki bonyeza hapa.

Zaidi ya kusoma kitabu tajwa hapo juu,endelea kufuatilia makala katika mtandao huu ambapo utapata maarifa yatakayokusaidia kufikia mafanikio katika nyanja mbalimbali za maisha. Unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala moja kwa moja kwenye email yako.

Kujiunga na mtandao huu bonyeza hapa au jaza fomu iliyopo hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *