Hizi Ndizo Sababu Kwa Nini Watu Hutafuta Utajiri Kwa Njia za Kishirikina

Mpenzi msomaji,

Tunaendelea na mfululizo wa makala kuhusu uhusiano wa ushirikina na mafanikio ya kiuchumi. Katika makala yaliyopita tuliona kwa nini waganga wanaweza kuwapatia watu wengine dawa au mbinu za kuwa matajiri wakati wao ni masikini. Na pia tuliangalia jinsi ambavyo unaweza kutumia mbinu wanazotumia waganga hao bila ya wewe kuwa mshirikina na ukafikia mafanikio makubwa yakiwemo mafanikio ya kiuchumi.

Kusoma makala ya nyuma bonyeza hapa

Katika makala ya leo, tutaangalia kwa nini watu wengi wakiwemo watanzania wanaamini kuwa ushirikina unaweza kuwaletea mafanikio. Tutaangalia pia nini tunaweza kufanya kujiepusha na imani hizo.

Zipo sababu nyingi kwa nini watu wengi wakiwemo watanzania wanaamini katika uchawi. Lakini kwa leo tutaangalia sababu kubwa sita tu:

Kukosa imani kwa Mungu

Imani za kweli za dini zinawafundisha watu kuwa Mungu ana uwezo wa kufanya mambo makubwa kwa wanaomwamini. Imani hizo huwajengea matumaini waumini  kuwa wakimtegemea Mungu atawawezesha kufanya mambo makubwa. Imani zote za kweli zinafundisha kuwa Mungu ana nguvu kuliko nguvu zingine. Kwa mfano, wakristo wanaamini na kufundisha kwamba uwezo wa  Mungu uko “juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia” (Waefeso 1:21). Hivyo, mtu yeyote anayeamini katika imani katika fundisho hili, hawezi kuamini katika nguvu za ushirikina. Lakini kwa kuwa watu wengi hawamwamini Mungu wa kweli, wanajikuta wanaamini katika ushirikina.

Hali ngumu ya maisha na kukosa matumaini

Kutokana na hali ngumu ya uchumi, watu wengi wamekuwa wako tayari kufanya chochote kinachowawezesha kupata fedha. Na pia kutokana na wananchi kukosa matumaini ya kwamba wanaweza kupata mafanikio kama watafanya kazi kwa bidii na maarifa imefanya watu wengi kuamini imani  za kishirikina ndio msaada kwao.

Mila na desturi

Kwa muda mrefu, katika jamii nyingi za watanzania kumekuwa na mila na desturi za ibada za matambiko. Hivyo, mtu anaingiziwa mawazo haya tangu akiwa mtoto mdogo na anakua akiamini hivyo. Kutokana na athari za imani za kichwani tangu utotoni hata mazungumzo ya kawaida yanatumia mifano na vielelezo vya kishirikina. Si ajabu mtu kutumia neno mchawi kumsifia mtu kwa kufanya vizuri jambo fulani. Kwa mfano, mtu anayeweza vizuri somo la Hisabati anaweza kuitwa “mchawi” wa Hisabati na mtu anayecheza vizuri mpira anaitwa “mchawi” wa mpira!

Ukosefu wa elimu sahihi

Kuendelea kuwa na imani potofu ikiwemo imani za kishirikina kunachangiwa na ukosefu wa elimu sahihi hasa ya kujitambua. Kuna watu wenye elimu za vyuo vikuu ila bado wanakwenda kwa waganga wapate mafanikio. Watu hawa wamekosa elimu ya kujitambua wao wenyewe na kuweza kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yao. Hii inawafanya watu kuwa watumwa wa imani hizi za kishirikina.

Ukosefu wa nidhamu binafsi

Kukosa nidhamu binafsi huenda ndilo tatizo kubwa kuliko yote. Watu wengi sana hawana nidhamu binafsi na hivyo hushindwa kujiongoza na kuvumilia vikwazo ili kufikia mafanikio yanayoyataka. Kwa mfano, watu wengi wanapopata fedha huwa hawawezi kupanga bajeti na kuifuata. Badala yake wanatumia pesa kiholela hadi zinapoisha ndipo wanagutuka kuwa kuna mambo muhimu walipaswa kufanya kwa pesa hiyo lakini wameshindwa.Huu ni ukosefu wa nidhamu binafsi. Watu hawa wanapokwenda kwa waganga na kupewa masharti huyaamini ni ya kweli na kushindwa kuelewa kwamba wanatengenezewa nidhamu binafsi ambayo wangeweza kutengeneza wenyewe.

 Hadithi za mitaani na vijiweni

Kitu kingine kikubwa kinachofanya watu wengi waamini imani za kishirikina ni hadithi ambazo wamekuwa wakizisikia. Hadithi hizi zinaweza kuwa zimetengenezwa au mtu kazipata kutoka kwa watu wengine na kuendelea kuzisambaza. Kwa mfano, siku hizi kuna habari za freemason, ambazo zimekuwa zikipewa nafasi hata kwenye vyombo vya habari. Hizi ni habari za upotoshaji ila zinaendelea kusambaa.

Mfano mwingine ni zile hadithi za kupokea. Kwa mfano, mtu anakuambia huko Kigoma kuna mganga anafufua wafu. Asilimia kubwa sana ya watu wanaamini hivyo japokuwa hawajawahi kuona. Au mtu anakuambia kule Sumbawanga mtu anaweza kukutumia radi, kitu ambacho sio kweli bali mazingira ndio yanayochangia.

Ufanye nini ili uweze kufikia mafanikio makubwa bila ya kutumia uchawi?

Ukifanya mambo yafuatayo unaweza kufikia mafanikio makubwa bila kutumia uchawi:

  1. Mwamini Mungu wa kweli na umtegemee na kumtanguliza katika mambo yako yote. Amini kuwa inawezekana kabisa kufikia mafanikio makubwa bila ya kutumia uchawi au kwenda kwa waganga.
  2. Tambua kwamba una uwezo mkubwa ndani yako na kwamba wewe ni wa pekee na una ubunifu na vipaji vingi sana. Jitambue na vijue vipaji hivyo na uanze kuvitumia kufikia mafanikio makubwa.
  3. Weka malengo na mipango ya maisha yako na ni mafanikio gani unataka kufikia.
  4. Jifunze kila siku kuhusiana na kile unachofanya. Pia soma sana vitabu mbalimbali vya kukuhamasisha na kukuongezea ujuzi na imani. Katika vitabu unavyosoma, kitabu cha kwanza kiwe Biblia.
  5. Fanya kazi kwa juhudi na maarifa. Tumia akili nyingi sana unapofanya kazi yako na pia fanya kazi zaidi ya watu wengine.
  6. Jenga nidhamu binafsi. Hii ndio itakayokuwezesha wewe kuendelea kusonga mbele hata kama mambo yamekuwa magumu. Nidhamu binafsi ndio uchawi wako utakaokupatia chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa. Najua unaweza na kama ukizingatia haya utafikia mafanikio makubwa sana.

Je, unataka kupata makala endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?

Basi unaweza kujiunga na mtandao huu ili uwe unapata makala kupitia email yako kila yanapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *