Nendeni chuoni mkijua hakuna ajira na mliofeli pambaneni na hali zenu.
Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Wiki iliyopita, Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), lilitangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha sita iliyofanyika Mei, 2023. Kama ilivyo kawaida, katika mitihani, wapo waliofaulu vizuri na kupata sifa za kuendelea na masomo ya elimu ya juu na wapo ambao ufaulu wao hautoshi kuendelea na masomo ya elimu ya juu. Matokeo ya kila mmoja yanatoa mwelekeo wa mustakabali wake. Nimeamua kuwaandikia waraka ili kuwashauri wahitimu hao hatua za kuchukua ili kuandaa mustabali wa maisha yao.
Nianze kwa kuwapongeza wahitimu wote kwa hatua hiyo kubwa mliyofikia kwenye maisha yenu bila kujali umefaulu vizuri au la. Hiyo ni hatua kubwa sana katika maisha yako. Kati ya mlioanza nao darasa la kwanza, ni wachache mliofanikiwa kufika kidato cha sita. Hivyo una kila sababu ya kupongezwa.
Kwa mliofaulu, mnaenda kusoma nini chuoni na kwa nini?
Siku moja baada ya matokeo ya kidato cha sita kutoka, niliombwa ushauri na mzazi mmoja ambaye mtoto wake amehitimu na amepata ufaulu wa juu sana. Mzazi huyo aliomba ushauri juu ya fani gani mtoto wake asome. Swali la kwanza nililomuuliza ni mtoto mwenyewe anapenda kusoma nini? Kilichonishangaza ni kwamba, mtoto mwenyewe hajui ni kitu gani anapenda kusoma bali chochote atakachoshauriwa atapokea!
Sitaeleza ni ushauri gani nilimpatia mzazi wa mtoto yule lakini ninachotaka kusema tu ni kwamba watoto wa aina hii ni wengi. Watoto wengi waliohitimu kidato cha sita hawajui nini cha kusoma katika elimu ya juu. Wapo wanaosubiri washauriwe na wazazi, walimu, ndugu, jamaa na marafiki na wengine watajaza kozi yoyote tu na kusubiri Tume ya Vyuo vikuu (TCU) iwachagulie.
Swali la ni kozi gani nzuri ya kusoma, kwa sasa lina majibu tofauti na ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita. Miaka ya nyuma fani za Sayansi kama uhandisi na udaktari wa binadamu zilionekana kuwa bora kutokana na uhakika wa kupata ajira na pia zilikuwa na kipato kizuri kulinganisha na fani zingine.
Lakini kwa sasa mambo yamebadilika, ajira sasa ni tatizo na kwa sababu hiyo hakuna tena fani ambayo ina uhakika wa ajira. Leo watu wanamaliza na kufaulu vizuri katika fani za uhandisi na udaktari lakini wanakaa miaka mingi bila kupata ajira. Na hata wale wachache wanaobahatika kupata ajira, hawapati mishahara mizuri kama miaka ya nyuma.
Kutokana na hali ya sasa, suala la fani gani inalipa au ni rahisi kupata ajira halipo tena. Hivyo, badala ya kuhangaika kuchagua ni fani gani ina uhakika wa ajira na kipato kizuri, wahitimu chagueni fani ambayo inaendana na vipaji vyako au vitu unavyovipenda. Hii ndiyo itakuwa fani bora kwako, kwa sababu utaziona fursa nyingi na nzuri pale utakapohitimu. Unaweza kuitumia fani hiyo kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.
Pengine, changamoto kubwa ni kwamba watu wengi hawajui vipaji vyao. Huenda hata wewe ukawa mmoja wao. Katika jamii zetu, hakuna mkazo katika kuwasaidia watoto kutambua na kutumia vipaji vyao. Matokeo ya hili ni kuwa watu wengi husomea fani ambazo haziendani na vipaji vyao au vitu wanavyopenda kufanya na hii inapelekea watu wengi kufanya kazi wasizozipenda. Kama wewe ni mmoja wa watu wa aina hiyo, endelea kufuatilia makala katika safu hii ili uweze kusoma makala zinazoweza kukusaidia kutambua kipaji chako na namna unavyoweza kunufaika nacho.
Kwa mliofeli, pambaneni na hali zenu
Kwa wahihitimu ambao ufaulu wenu hauwawezeshi kuendelea na elimu ya juu, siwapi pole bali narudia tena kuwapongeza kwa hatua hii mliyofikia. Inawezekana umeumia sana kwa kupata matokeo hayo uliyopata maana hakuna anayefanya mtihani ili apate ufaulu mdogo. Hata hivyo, naomba niwaambie kuwa kufeli shule siyo kufeli maisha. Ninakutia moyo upambane na hali yako. Huu ndiyo wakati ambao unahitaji kufanya maamuzi muhimu sana kuhusu maisha yako. Huenda ulitegemea uendelee na masomo ya elimu ya juu lakini imeshindikana kwa sasa. Hivyo, unahitaji kukaa chini na kuamua ufanye nini kwa mustakabali wa maisha yako.
Kama bado una mpango wa kuendelea na elimu ya juu, usikate tamaa maana unaweza kufikia ndoto yako hiyo bila kujali kuwa umefeli mtihani kwa sasa. Unaweza kuamua kurudia mitihani au kutumia cheti cha kidato cha nne kusoma fani uitakayo kwa ngazi ya cheti na baadaye ukajiendeleza hadi ngazi ya shahada ya chuo kikuu.
Kama utaamua kuachana na elimu ya darasani na kuanza maisha, bado utakuwa ni uamuzi sahihi pia. Anza sasa kujitengenezea kipato kwa kuchagua ni njia ipi utakayotumia, ni maarifa yapi ya ziada unayohitaji na ni thamani gani ambayo upo tayari kutoa kwa wengine. Fanya haya sasa, usiendelee kupoteza muda wako kufikiria kwa nini umefeli mtihani, badala yake shika hatamu ya maisha yako na anza kuweka juhudi kwenye lile eneo ambalo umechagua kuchukua hatua. Kwa kifupi, anza mara moja kupambana na hali yako.
Waraka huu utaendelea. Endelea kufuatilia.
Je, unataka kupata makala endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?
Basi unaweza kujiunga na mtandao huu ili uwe unapata makala kupitia email yako kila yanapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.