Baada ya kudanganywa na kijidanganya, huu hapa ukweli ambao huujui
Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Hiki ni kipindi cha mwaka ambacho wanafunzi wa elimu ya juu (isipokuwa wachache) wamekamilisha muhula wa mwisho wa mwaka wa masomo. Na kati yao kuna ambao wamehitimu masomo yao kwa ngazi mbalimbali kuanzia astashahada (certfificate), stashahada (Diploma), shahada ya kwanza (undergraduate degree) na hata shahada za juu (postgraduate degrees).
Nimeamua kuandika waraka kwa wahitimu wa elimu ya juu ili kuwakumbusha kama siyo kuwafungua macho juu ya hali halisi watakayokabiliana nayo baada ya kumaliza masomo yako kwa maana wamedanganywa sana na kudanganyika. Huu ni mwendelezo wa makala ambapo nilianza na wahitimu wa kidato cha sita katika makala yaliyopita na leo ni zamu ya wahitimu wa elimu ya juu.
Nianze kwa kuwapongeza wahitimu wote kwa hatua hiyo kubwa mliyofikia kwenye maisha yenu. Kwa wale mliohitimu shahada ya kwanza mtakuwa mmetumia si chini ya miaka 18 kuanzia elimu ya awali hadi sasa. Kati ya mlioanza nao elimu ya awali, wewe ni kati ya watu wachache sana mliofanikiwa kufika hatua hii. Hivyo una kila sababu ya kupongezwa. Pamoja na pobgezi hizo nasikitika tu kukuambia kuwa kwa miaka 18 au zaidi ya safari yako ya elimu, kuna mengi umedanganywa, ukadanganyika. Zaidi ya kudangwa na kugandanyika, wewe pia umejidanyanga!
Umedanganywa nini?
Pamoja na kazi kubwa uliyofanya ya kusoma kwa juhudi kubwa, kuna kitu kimoja mpaka sasa huenda hujakijua kuwa umekuwa ukidanganywa. Nasema umedanganywa kwa sababu vitu ambavyo umekuwa unaambiwa kwa miaka hiyo 18 havifanyi tena kazi au havipo na vimeshapitwa na wakati.
Kuanzia katika familia hadi jamii kwa ujumla kulikuwa na wakati mzuri sana wa kukupa ushauri kwamba soma kwa bidii, faulu vizuri na utapata kazi nzuri na kuwa na mafanikio. Zipo kauli nyingi zilizotengenezwa kuelezea suala hili kama vile elimu ni ufunguo wa Maisha, elimu ni siri ya mafanikio, Soma Ule na kauli zingine. Walimu waliokufundisha kila ngazi walikuwa wanakuimbia wimbo huo huo kila mwaka na ulipofika chuoni wahadhiri wako nao waliuendeleza wimbo huo tena kwa sauti kubwa zaidi.
Jamii na walimu wako watakuwa wamekupa hadithi nzuri sana za watu waliosoma na wakawa na mafanikio makubwa. Na pia watakuwa wamekupa hadithi nzuri sana za watu ambao kwa sababu moja ama nyingine hawakusoma na maisha yao yakawa mabovu. Tatizo ni kwamba walikuwa wanasisitiza hapo tu na hawakuongelea upande mwingine wa shilingi ambao una watu wengi zaidi ya hao waliowataja. Kuna watu wengi waliosoma ila maisha yao ni magumu sana na kuna watu wengi ambao hawajasoma au wamesoma kidogo tu lakini maisha yao ni ya mafanikio kuzidi wenye elimu kubwa zaidi yao.
Umedanganywa kwa sababu ulimwengu wa kazi nzuri zenye kuleta mafanikio uliokuwa unahubiriwa kwa sasa umeshapotea. Kama huniamini siku chache zijazo utalishuhudia hili kwa uchungu sana. Katika makala yanayofuata nitaeleza zaidi kuhusu hili.
Mmedanganyana Nini?
Licha ya kudanganywa, wewe na wanafunzi wenzako pia mlidanganyana pia. Kuna hadithi nzuri sana huwa zinazunguka kwenye karibu kila chuo Tanzania hii na hata nje ya Tanzania. Hadithi hizo ni kwamba “Nikimaliza chuo nitapata kazi kwenye ofisi fulani, nitakuwa nalipwa milioni kadhaa, nitakopa gari na kupanga nyumba sehemu fulani wakati najipanga kujenga ya kwangu”. Hongereni kwa ndoto hizo nzuri. Tatizo tu ni kwamba hicho mlichokuwa mnakiota hakipo. Kwa kifupi ni kwamba hizo mlizokuwa mnaambizana ni hadithi. Uhalisia hauko hivyo.
Mliendelea kudanganyana kwa kuangalia watu wachache waliowaacha chuoni ambao mambo yao yamekuwa mazuri. “Umemuona Musa, amemaliza kozi hii niliyosoma mwaka juzi na sasa ameajiriwa kwenye kampuni kubwa na analipwa vizuri sana, tayari ana gari na nyumba.”
Hongera sana kwa kuwa mfuatiliaji mzuri wa waliokutangulia, lakini tatizo ni moja hapa, mbona unawafuatilia wachache sana ambao ndio wamefikia viwango hivyo ulivyotaja hapo. Vipi kuhusu darasa zima la akina Musa, unakumbuka wale wenzake waliosoma kozi hiyo wako wapi? Vipi kuhusu waliomaliza kozi hiyo na nyingine nyingi kwenye vyuo vingine? Wako wapi? Ni vyema ukaacha kuangalia wachache sana waliofikia mafanikio na kuangalia pande zote ili kupata ukweli halisi wa mtaani.
Kuna vitu vingi sana ambavyo umedanganywa na wewe ulikuwa unadanganyana na wenzako. Sasa unapata nafasi ya kuingia mtaani kwenda kuona uhalisia wa mambo, sitaki kukutisha kwamba mambo yatakuwa magumu. Ninachoweza kukuambia tu ni kwamba nenda mtaani ukajifunze upya maana halisi ya Maisha ya mafanikio.
Kama ukiweza kutengeneza maana mpya ya mafanikio utaishi maisha yenye mafanikio na utakayoyafurahia. Kama utasubiri jamii ndiye ikupatie maana yake ya mafanikio utaishi maisha ya mbio za panya katika maisha yako yote ambayo Mwenyezi Mungu atakujalia kuishi hapa duniani. Ni maana ipi ya mafanikio unaweza kuitengeza na utaitengeneza kwa namna gani? Endelea kufuatilia makala katika mtandao huu, utaweza kuelewa hili.
Najua wazo ulilo nalo baada ya kumaliza masomo ni kutafuta ajira maana ndivyo ulivyodanganywa,ukadanyika na kujidanganya. Katika makala ya yanayofuata nitakupatia mambo muhimu ambayo unapaswa kuyajua kabla ya kuanza kuzunguka na bahasha ya kaki kutafuta ajira. Endelea kufuatilia.
Je, unataka kupata makala endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?
Basi unaweza kujiunga na mtandao huu ili uwe unapata makala kupitia email yako kila yanapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.
Ubarikiwe Sana