Kabla ya Kuzunguka na Bahasha Kusaka Ajira, Nina Ujumbe Wako
Rafiki yangu mpendwa,
Karibu tena mpenzi msomaji katika mwendelezo wa waraka wa wazi kwa wahitimu wa elimu ya juu 2023. Katika makala yaliyopita niliwaonesha namna ambavyo mmekuwa mkidaganywa na kudanganyana kuhusu maisha baada ya masomo yenu hususani kuhusu upatikananji wa ajira na mishahara mizuri. Ukweli niliowaeleza ni kwamba ajira mlizokuwa mnaambiwa kuwa mtazipata hazipo na hata ukibahatisha kuzipata mishahara si mikubwa kama mlivyokuwa mnadanganyana.
Kusoma makala ya nyuma, fungua hapa
Pamoja na kuwapa ukweli huo, nina hakika bado mna mawazo ya kutafuta ajira katika fani mlizosomea maana waswahili walisema kusikia kwa kenge mapaka damu itoke puani. Na wewe huenda unasubiri damu itoke puani ndipo usikie kwamba nilichokueleza ni kweli.
Wazo la kutafuta ajira siyo baya na sisemi msiwaze kabisa kuajiriwa maana ndicho mlichoaandaliwa kufanya. Elimu yenu imewaandaa kuajiriwa katika fani uliyosomea. Yaani, kama umesomea ualimu inabidi utafute kazi ya ualimu na kama umesomea udaktari inabidi utafute kazi ya udaktari. Kwa hiyo, kubadilisha kile kilichoingizwa vichwani mwenu kwa miaka mingi siyo kazi rahisi.
Bila shaka, wengi wenu mmeshatoa nakala za kutosha za vyeti na kuandaa wasifu (CV) ili muanze kuzunguka na bahasha kupeleka katika ofisi mbalimbali kuomba nafasi ya ajira. Kabla hujaweka nguvu na matumaini yako kwenye mchakato wa kuzunguka na bahasha kuna vitu vichache ambavyo ni vyema ukavijua. Vitu hivyo ni kama ifuatavyo:
1. Nafasi za ajira ni chache kuliko idadi ya wahitimu wenye sifa. Kwa sasa karibu kila kada kuna nafasi chache sana serikalini na hata kwenye taasisi binafsi. Hivyo, unavyoingia mtaani yakupasa ujue ukweli huu.
2. Sio kila nafasi za kazi zinazotangazwa ziko wazi. Kuna baadhi ya taasisi zinatangaza nafasi za kazi ili tu kutimiza sheria na taratibu za ajira zinazotaka nafasi za kazi zitangazwe kwa umma lakini kuna watu tayari walishaandaliwa. Hivyo, unaweza kuandika maombi, ukaitwa kwenye usaili na bado ukaambiwa umekosa nafasi.
3. Jifunze kutoka wahitimu waliokutangulia: Wahitimu wenzako wa mwaka jana na mwaka juzi bado wanazunguka na bahasha mtaani. Kuna ambao bado wanaendelea kupitisha bahasha na kuna baadhi ambao wameamua kufanya mambo mengine. Ni vyema kuwatafuta wa kila kundi ili ujifunze machache kutoka kwao.
4. Mishahara ya kazi za kwenye taasisi binafsi ni midogo sana. Tofauti na hadithi za vyuoni kwamba mishahara kwa wahitimu wa shahada ni mikubwa ukweli ni kwamba kuna wahihitmu wa shahada kama wewe wanalipwa mshahara wa chini ya laki tatu. Kama ukipata kazi na mshahara wakakutajia mdogo kama huna kingine cha kufanya ni bora kuchukua kazi hiyo ila uifanye kwa lengo la kupata ujuzi na kujenga mtandao na watu wanaofanya kada uliyosomea. Badala ya kukaa miaka ukizunguka na bahasha ukitegemea mshahara mkubwa ni bora kupata japo huo mshahara mdogo kwa mwezi huku ukiendelea kukuza mtandao wako na ujuzi wako.
5. Fanya kazi za kujitolea. Ikitokea umekosa hata kazi ya mshahara mdogo, kuna ofisi nyingi ambazo zina mpango wa watu kujitolea kufanya kazi na baadaye unaweza kuingizwa kwenye ajira. Kama kuna namna ambayo unaweza kupata pesa ya kula na nauli, fanya kazi za kujitolea na huko onesha uwezo wako na vipaji vyako. Kwa kuonesha uwezo na vipaji itakuwa rahisi kukubalika na kupewa nafasi, na pia utatengeneza mtandao wa watu watakaokuonesha njia zaidi.
6. Usichague kazi: Upo msemo wa Kiswahili unasema mfungwa hachagui gereza. Kwa kuwa nafasi za jaira ni chache, basi nawe jiweke katika nafasi ya mfungwa. Si lazima ufanye kazi ya kitu ulichosomea. Kuna baadhi ya kazi zinaweza kufanywa na mtu yeyote aliyehitimu elimu fulani. Kwa mfano, unaweza kutafuta shule na ukafundisha masomo yanayohusiana na ulichosomea. Kama umesoma kada za biashara unaweza kufundisha masomo ya biashara, kama umesoma sayansi kuna nafasi kubwa za kufundisha masomo ya sayansi kutokana na uhaba wa walimu wa Sayansi katika shule nyingi. Kama unadhani kushika chaki sio hadhi yako basi endelea kuzunguka na bahasha mjini.
7. Tengeneza ajira yako mwenyewe: Angalia ni kitu gani unachoweza kufanya katika mazingira unayoishi ilim kutengeneza ajira badala ya kuendelea kutafura ajira. Elimu inapaswa kukuandaa kupambana na mazingira yako. Hii ndio dhana halisi ya elimu. Lakini kwa bahati mbaya, elimu ya darasani haituandai kwa hilo. Elimu hiyo inatuandaa kuwa waajiriwa basi tunajikuta wote tunasubiri kuajiriwa. Ni vyema ukaanza kufikiri tofauti na uliyofundishwa chuoni kuhusu ajira.
Namna nzuri ya kutengeneza ajira yako mwenyewe ni kujiajiri. Ni vema ukafikiria kujiajiri na pengine ndicho ingebidi kiwe kitu cha kwanza mawazoni mwako. Kama utachoshwa na kuzunguka na bahasha mtaani ama kama hutaki kupata hiyo karaha ni vyema ukafanya maamuzi ya kutotegemea kuajiriwa. Tumia uwezo na vipaji ulivyonavyo, changanya na elimu uliyoipata halafu tumia mazingira yako kutengeneza ajira kwako na kwa watu wengine.
Katika makala yajayo ijayo nitakueleza kwa kifupi ni wapi unaweza kuanzia katika safari yako ya kujiajiri. Endelea kufuatilia.
Je, unataka kupata makala endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?
Basi unaweza kujiunga na mtandao huu ili uwe unapata makala kupitia email yako kila yanapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.