Rafiki yangu Mpendwa,
Je, umewahi kuhisi kutosikilizwa kwenye mazungumzo ya aina yoyote? Labda ulikuwa katikati ya kuzungumza, mtu fulani akakukatiza kabla hujamaliza, au labda ulimaliza kuzungumza ukitegemea kujibiwa ukakutana na ukimya wa kushangaza na ukagundua kuwa mtu uliyekuwa unaongea naye alikuwa anachati kwenye simu na hivyo alikuwa hakusikilizi? Je, ulijisikiaje?
Katika mazungumzo ya aina yoyote, yawe baina yetu na marafiki, wenzi wetu wa ndoa, wafanyakazi au wafanyabiashara wenzetu, wanajamii wenzetu na kadhalika, ustadi wa mawasiliano yenye ufanisi ni muhimu kwa mafanikio na uhusiano mwema.
Hata hivyo, wengi wetu, bila kujua, huwa tunajikuta tunaonesha tabia mbaya za mawasiliano ambazo zinaweza kuzuia maingiliano na mahusiano yetu. Matokeo yake tunaishia katika migogoro na kuharibika kwa mahusiano kuanzia katika ndoa, familia, jamii na katika maeneo ya kazi.
Katika zama hizi ambazo mawasiliano mengi yanafanyika kidigitali, uwezo wa kufanya mazungumzo mazuri unaelekea kupotea kwa watu wengi. Hii inasikitisha lakini ni kweli. Uwezo wa kufanya mazungumzo mazuri na yenye tija unaonekana umebaki katika matukio rasmi tu kama vile kwenye vikao rasmi vya ana kwa ana. Tofauti na hapo ni changamoto.
Siku hizi, si ajabu kuona, kwa mfano, wanafamilia wameketi kwenye meza ya chakula yenye vyakula vitamu lakini kila mmoja wao ameinamisha kichwa chake akiwa ameshika kijiko au uma katika mkono mmoja huku mkono mwingine akiwa ameshikilia simu au kishikwambi akiendelea kuongea, kuchati au kusoma kitu fulani. Na wakati huo huo ndani ya chumba hicho kuna radio au televisheni imewashwa kwa sauti ili watazame na/au kusikiliza. Katika mazingira hayo, watu hawa wako pamoja kimwili lakini kiuhalisia hawako pamoja na hawawezi kuwa na mazungumzo ya maana.
Rafiki yangu mpendwa, mazungumzo yako na wengine yanaweza kuwa ya kufurahisha, yenye faida kwako, yenye kujenga au yanaweza kuudhi au yanaweza kuwa ya kupoteza muda na hata kuishia kwenye ugomvi. Kwa vyovyote vile itakavyokuwa, tabia zako wewe na tabia za mtu unayezungumza naye ndiyo zitaamua jinsi mazungumzo yenu yatakavyokuwa.
Ili uweze kuwa na mazungumzo yenye tija na ya kufurahisha pande zote mbili, unapaswa kuacha baadhi ya tabia zisizofaa ili usiharibu mazungumzo na hata uhusiano wako na watu wengine. Ukiwa na tabia hizo huenda watu wakaepuka kuzungumza nawe na unaweza kujipatia sifa ya kuwa mtu asiye na heshima na anayepuuza waziwazi wengine. Huenda unafanya hivi bila kukusudia, kwa hivyo tafadhali fuatilia makala haya kwa makini ili kuhakikisha unaacha tabia hizi mbaya.
Baadhi ya tabia mbaya katika mazungumzo ni hizi zifuatazo:
Kukatiza watu
Mazungumzo hutiririka vizuri wakati wazungumzaji wanapozungumza kwa zamu. Kumkatiza mtu anapozungumza kunavuruga mtiririko huo na kunaonyesha kutokuheshimu mawazo na hisia za mzungumzaji.
Unapoendelea kumkatiza mtu, anaweza kusahau anachotaka kusema au anakuachia wewe peke yako. Kukatiza mazungumzo kila mara kunaweza kumfanya mtu unayemkatiza ajisikie vibaya na wakati mwingine apate hasira na asiwe tayari kuendelea na mazungumzo. Kuwa msikilizaji mzuri ni muhimu sana katika mahusiano kama vile ndoa, urafiki na mahusiano ya kikazi. Jitahidi kuwa mvumilivu na uwaruhusu wengine wamalize kuongea kabla ya wewe kuongea.
Inaeleweka, kuna nyakati unaweza kuhisi ni muhimu kukatiza. Waandishi wa habari hufanya hivi mara kwa mara. Kwa mwandishi wa habari, inaweza kuwa muhimu kukatiza ili kuhakikisha hoja zote anazohitaji zingumzwe zimezungumzwa zote.
Katika mazungumzo ya kawaida, inaweza kuwa sahihi kumkatiza mtu katika mazingira fulani fulani. Kwa mfano, ikiwa unataka kusahihisha kwa haraka kitu alichosema kimakosa na unadhani kitaathiri hoja zake au kama unataka azungumzie suala jipya ambalo limejitokeza akilini mwako na litamsaidia katika hoja zake. Pia, unaweza kumkatiza kwa sababu ya muda.
Iwapo ni muhimu kumkatiza mtu kwa sababu muhimu, usifanye hivyo wakati yuko katikati ya sentensi au hoja fulani. Badala yake msubiri amalize sentensi au hoja yake ndipo umkakatize. Unapofanya hivyo ni muhimu kumuomba radhi na kumueleza sababu ya kumkatiza.
Mawasiliano yenye ufanisi ni njia ya pande mbili (two-way traffic) lakini kwa bahati mbaya hilo halitokei kila wakati kwa sababu ya tabia mbaya ya kukatizana. Sababu moja wapo ni kwamba watu wengi si wasikilizaji makini. Biblia inasisitiza sana suala la kuwa msikilizaji makini. Kwa mfano, katika Yakobo 1:19 Biblia inasema “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika”. Na Mithali 18:13 inasema “Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake.”
Kusikiliza kwa umakini si kungoja tu zamu yako ya kuzungumza; bali ni kujaribu kwa dhati kuelewa kile ambacho mtu mwingine anazungumza. Kusikiliza kwa makini kunahusisha zaidi ya masikio yetu tu. Kutazamana macho na kutikisa kichwa mara kwa mara, yote yanaonyesha usikivu. Vidokezo hivi visivyo vya maneno huonyesha mzungumzaji kuwa tunahusika na tunavutiwa. Fikiria kisa cha Zakayo katika Luka 19:1-10, mtoza ushuru aliyetengwa na jamii yake. Yesu anapomtafuta na kujialika nyumbani kwa Zakayo, andiko hilo halitaji maneno yaliyosemwa, lakini kitendo cha Yesu kusimama na kumwangalia Zakayo kinadokeza kupendezwa kwa kweli na mtu huyo, kikitayarisha njia kwa ajili ya kukutana na kuleta mabadiliko kwake.
Kukamilisha Maneno au Sentensi za Wengine
Baadhi ya watu wengine wana tabia isiyofurahisha ya kukamilisha sentensi za wengine. Ndiyo, kuna wakati inaweza kuwa muhimu kumalizia maneno ya mtu. Kwa mfano, ikiwa mtu anatafuta neno sahihi la kuongea au amesahau neno au jambo fulani kama vile jina la mtu, tarehe ya tukio fulani na kadhalika. Hapo haitakuwa vibaya ukimalizia neno au sentensi yake. Lakini wapo watu ambao wana kawaida ya kumalizia kila neno au sentensi za watu wengine.
Mazungumzo na watu wa aina hii yanaweza kuudhi sana kwa sababu wataingilia mazungumzo yako na wanaweza kukupotezea mwelekeo wa mazungumzo. Na wakati mwingine wanaweza kukufedhehesha au kukudhalilisha bila sababu. Hebu fikiria, wewe una kigugumizi halafu unaongea na mtu anayependa kukamilisha maneno au sentensi za wengine. Hayo mazungumzo yatakuwaje? Bila shaka yatakuwa mazungumzo yenye kuudhi na kufedhehesha.
Unapokuwa katika mazungumzo, waache watu unaozungumza nao wamalizie maneno au sentensi zao wao wenyewe. Usiwapangie maneno. Waache wawe huru kutumia maneno kama wanavyotaka wao. Hapo ndipo mazungumzo yatakuwa matamu.
Ukiacha watu wanaomalizia maneno ya watu wengine, kuna watu ambao hawakamilishi sentensi au maneno bali huwaachia watu wanaoongea nao wakamilishe. Hii nayo ni tabia mbaya. Kama ambavyo haipendezi kukamilisha maneno ya watu wengine, hali kadhalika, unapoongea usitengeneze mazingira kwa mtu mwingine kukamilisha maneno au sentensi zako. Kamilisha maneno au sentensi zako mwenyewe.
Kwa leo naomba tuishie hapa. Tutaendelea na tabia zingine katika makala yanayofuata.
Kama hujajiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini ili uweze kupokea makala kwenye barua pepe yako moja kwa moja.