Unapopiga Kura Katika Uchaguzi wa Leo, Usisahau Kujipigia Kura Wewe Mwenyewe hata Kama Hujagombea

Rafiki yangu mpendwa,

Leo ni siku muhimu kwa Watanzania—Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Wananchi wanachagua viongozi wa vijiji, mitaa, na vitongoji, wakiwemo wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa. Kama viongozi mbalimbali walivyosisitiza, uchaguzi huu una umuhimu mkubwa kwa maendeleo yetu. Kwa hiyo, tunapaswa kujitokeza kwa wingi na kutumia haki yetu ya kikatiba kuwachagua viongozi bora watakaosaidia kuchochea maendeleo ya maeneo yetu.

Natoa wito kwa kila aliyejiandikisha kupiga kura kuitumia haki hii muhimu. Mimi tayari nimeshapiga kura, nikichagua viongozi ninaoamini wanafaa. Hata hivyo, kuna jambo moja la ziada ambalo nataka ulizingatie leo: jipigie kura mwenyewe hata kama hujagombea.Wanaoeleza kuwa viongozi wa serikali za mitaa ni muhimu kwa ajili ya kuleta maendeleo yetu hawasemi uongo lakini pia hawasemi ukweli. Najua hujanielewa. Endelea kusoma  ili unielewe.

Kwa nini hawasemi uongo?

Ni kweli kabisa kwamba viongozi wanawezq kuchangia kuleta maendeleo au kurudisha nyumba maendeleo yetu. Kwa kupiga kura katika chaguzi wa leo, utakuwa umechangia kuunda uongozi katika maeneo yako ambao wataweza kuleta maendeleo na kuboresha hali zetu za maisha au kinyume chake.

Kwa nini hawasemi ukweli?

Pamoja na ukweli kwamba viongozi wanaweza kuchangia kuleta maendeleo yetu lakini ukweli ambao wengi hawausemi ni kwamba viongozi wanatengeneza mazingira tu kwa ajili ya wananchi kujiletea maendeleo yao binafsi. Hata kama tutapata viongozi wazuri kiasi gani hawawezi kukuletea maendeleo yako binafsi ikiwa wewe hautakuwa tayari kuyatafuta maendeleo hayo. Lazima wewe mwenyewe ufanye uamuzi na kuchukua hatua ya kujiletea maendeleo yako binafsi ili uweze kufaidika na mazingira mazuri ambayo yataletwa na viongozi uliowachagua.

Kwa muktadha huo, napendekeza kuwa baada kupiga kura leo kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, rudi nyumbani ukatafakari ni namna gani utaweza kujiletea maendeleo yako binafsi. Baada ya kufanya uamuzi wa nani akuongoze kupitia sanduku la kura ili akuletee maendeleo, fanya uamuzi wa namna ya kuongoza maisha yako ili kujiletea maendeleo. Kwa maneno mengine,  baada ya kupiga kura  kumchagua kiongozi wako, ni muhimuuchague pia mtu mwingine ambaye si lazima awe mgombea katika uchaguzi wa leo ili akuongoze kuleta maendeleo yako binafsi. Mtu huyo muhimu unayepaswa kumchagua leo kama unataka maisha yako yabadilike ni wewe.

Rafiki, najua kampeni za kuomba nani achaguliwe zimefungwa jana. Lakini leo nataka nimpigie kampeni mgombea mmoja, ambaye ana nguvu kubwa ya kubadilisha maisha yako lakini hayupo kwenye karatasi za uchaguzi. Mgombea huyo ni “Wewe.”

Unapojichagua kuwa kiongozi wa maisha yako, ahadi zako zitakuwa rahisi kutekelezeka kwa sababu wewe ndiye utendaji mkuu. Hakutakuwa na visingizio vya “mchakato” au “upembuzi yakinifu” kama ambavyo viongozi wa kisiasa huwa wanasingizia,

Napendekeza hii ndiyo ahadi yako kwa maisha yako:

Mimi [taja jina lako], nimejichagua kuwa kiongozi wa maisha yangu. Maisha yangu ni jukumu langu, na nitahakikisha ninachukua hatua kuboresha kila siku. Nitajitahidi kuwa bora kuliko jana. Nitajifunza, nitajituma, na kuongeza thamani katika kila ninachofanya. Nitaweka sehemu ya kipato changu kwa akiba, na baadaye nitawekeza ili kipato hicho kizalishe zaidi. Sitawalaumu wengine kwa changamoto zangu. Badala yake, nitabadili ninachoweza na kuachana na kile ambacho siwezi kubadili. Haya ni maisha niliyoyachagua kwa miaka mitano ijayo.”

Mwandishi maarufu wa vitabu vya kikristo Ellen G. White anatufundisha kuwa:

Wale wanaojizatiti kwa maamuzi ya dhati ya kufanikisha maisha yao, wakimtegemea Mungu, hawatakosa njia za kufanikisha malengo yao.” (Steps to Christ, uk. 70). Hivyo, nawe ukimtegemea mungu katika maamuzi na mipango yako, Hapana shaka utafanikiwa.

Hapa sihitaji kukushawishi sana kumchagua mgombea anayeitwa “wewe”, kwani ninachotaka ufanye ni kujilinganisha ulivyo leo Novemba 2024 na ulivyokuwa Novemba 2019 ulipopiga kura kumchagua mgombea tofauti na “wewe”. Kama kuna chochote kimebadilika kwenye maisha yako, basi utaona wazi mabadiliko hayo yamechochewa na vitu viwili; kwanza mazingira mazuri yaliyowekwa na viongozi uliowachagua. Pili, juhudi zako binafsi. Bila juhudi zako binafsi huwezi kupata maendeleo yako binafsi hata kama una viongozi wazuri kiasi gani lakini unaweza kuwa na viongozi wasio wazuri lakini ukafanya juhudi kubwa za kujiletea maendeleo na ukatoboa.

Ninakushawishi ukubaliane nami  kuwa maendeleo yako binfasi kwa sehemu kubwa yanakutegemea wewe na siyo viongozi. Kwa sababu hiyo, ni muhimu unapowachagua viongozi, usiache kumchagua mgombea anayeitwa “wewe” maana usipomchagua huyo hata kuchagua viongozi wengine ni kazi bure.

Tatizo kubwa wakati wa mchakato wa uchaguzi wa viongozi hasa kwenye kampeni ni kuwa wengi wanaongea na kuahidi mengi na wengine wanahonga ili wapate nafasi wanazotaka. Wanapozipata sote tunajua ni nini kinatokea, hakuna kubwa linalobadilika na wakati mwingine mambo yanakuwa mabaya zaidi. Kwa kuangushwa huku tunahamishia matumaini yetu kwenye uchaguzi unaofuata kwamba “tutawakomesha kwenye uchaguzi ujao”.

Sasa, angalia na wewe utakapojichagua kuwa kiongozi wa maisha yako, usiongee maneno mengi bali fanya vitendo vingi maana hautakuwa na mtu wa kumkomesha katika uchaguzi mwingine maana huwezi kujikomesha wewe mwenyewe.

Baada ya kukupigia kampeni “wewe” ili ujichague kiongozi wa maisha yako, nakutakia ushindi wa kishindo na baada ya kushinda hakikisha unatekeleza hadi zako maana hauna wa kumkomesha katika uchaguzi ujao.

Mtandao huu wa Mkristo na maisha ya mafanikio ni jukwaa la kukuongoza kujifunza mengi kuhusu maendeleo binafsi, usimamizi wa fedha, ujasiriamali, mahusiano ya familia, na masuala ya kiroho. Kama umeamua kujichagua kuwa kiongozi wa maisha yako, hakikisha unafuatilia maarifa haya ili kusaidia safari yako ya mafanikio.

Ili kupata makala moja kwa moja kupitia barua pepe (e-mail) yako, jaza fomu iliyopo hapa chini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *