KITABU: SIRI ZA MAFANIKIO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA

SIRI ZA MAFANIKIO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA: KANUNI ZA KIBIBLIA NA KIUCHUMI ZA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO NA MIGOGORO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA

Tafiti zilizofanyika katika nchi mbalimbali zinaonesha kuwa mojawapo ya mambo yanayooongoza kusababisha migogoro na kuvunjika kwa ndoa ni fedha. Hata hivyo, ni vizuri ieleweke kuwa kinachosababisha migogoro ya ndoa siyo kukosa fedha wala siyo kuwa na fedha nyingi bali ni kukosekana kwa elimu ya msingi ya usimamizi wa fedha binafsi. Unaweza kuwa na fedha nyingi lakini kwa sababu hauna maarifa na elimu ya kusimamia fedha, ukajikuta unaingia katika migogoro ya kifedha.  Wapo wanandoa walioachana kwa sababu ya hali ngumu ya kifedha na wengine wameachana baada ya kuwa na fedha nyingi.  Kwa upande mwingine, kuna watu wengi wana ndoa zisizo na migogoro lakini wana maisha yenye changamoto za kifedha na vilevile wapo wanaoishi maisha mazuri ya ndoa wakati wana fedha nyingi.

Kitabu hiki kinakuja na suluhisho la changamoto za kifedha katika ndoa. Kwa ufahamu wa waandishi, hiki ni kitabu cha kwanza kwa lugha ya Kiswahili kinachohusu usimamizi wa fedha katika ndoa na familia kwa mtazamo wa Kikristo. Kitabu hiki kimeandikwa ili kuziba ombwe la elimu ya fedha kutokana na ukweli kwamba elimu ya fedha ni muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku hasa katika ndoa na familia lakini kwa bahati mbaya, elimu hii haifundishwi kwa usahihi katika mfumo wetu wa elimu na katika mafundisho ya kiroho makanisani.

Masomo yaliyomo kwenye kitabu hiki yako katika makundi makuu manne. Kundi la kwanza linajenga msingi wa masomo yote ambapo utajifunza umuhimu wa fedha katika ndoa na familia, njia mbalimbali za kusimamia fedha katika ndoa, sababu za migogoro katika ndoa na familia na namna ya kuiepuka au kukabiliana nayo.

Kundi la pili la masomo, linahusu matumizi ya fedha. Hapa utajifunza namna ya kudhibiti matumizi ya fedha zako kwa kupanga bajeti na kuifuata. Utajifunza mbinu mbalimbali zitakazokuwezesha kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha bila kulazimika kujibana na kuishi maisha magumu. Vilevile, kitabu kinaeleza namna ya kuokoa fedha yako kwa kuweka akiba na kukata bima mbalimbali kama njia ya kukabiliana na dharura na majanga yanayoweza kujitokeza. Eneo jingine muhimu katika sehemu hii ni suala la mikopo na madeni ambapo faida na hatari za madeni zimechambuliwa kwa kina na namna ya  kunufaika na mikopo na jinsi unavyoweza kuepuka hatari za madeni, mikopo ipi ya kuchukua na ipi ya kuepuka na namna unavyoweza kuishi bila madeni na ukawa na maisha bora.

Kundi la tatu la masomo, linahusu namna ya kujipanga kwa maisha ya mbele, yaani namna gani unaweza kujiandaa kwa ajili ya maisha bora baada ya kuzeeka au kustaafu. Suala la wosia na usimamizi wa mirathi limeelezwa na kufafanuliwa kwa ajili ya kukusaidia kuiacha familia yako bila migogoro ikiwa utafariki. Kundi la nne ni elimu ya fedha kwa watoto ambayo utajifunza namna ya kumfundisha mtoto wako elimu ya fedha ili kumuandaa aweze kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu dhana ya fedha, namna ya kuitafuta, kuisimamia na kuiongeza kwa namna inavyomtukuza Mungu ili elimu hii imuwezeshe kuwa na mafanikio ya kifedha katika maisha yake.

Kitabu hiki kinawafaa watu wote walioko kwenye ndoa, wanaotarajia kuingia kwenye ndoa na wanafamilia kwa ujumla. Kwa kifupi, kitabu hiki kinamfaa kila mtu. Kwa kusoma kitabu hiki utaweza kupata maarifa ambayo yatakusaidia kuwa na mafanikio ya kifedha katika ndoa au familia yako na kuepuka migogoro inayosababishwa na ukosefu wa elimu sahihi ya fedha.

Jinsi ya kupata kitabu hiki

Ili uweze kuelekezwa namna ya kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com